RIP: Aliyekuwa beki wa Harambee Stars Mark Odhiambo ameaga dunia

Aliripotiwa kufariki mwendo wa saa tano asubuhi ya Jumanne Desemba 27 baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Muhtasari

• Odhiambo aliziwajibikia timu kama Tusker, KCB,Wazito, Mathare miongoni mwa zingine enzi za uchezaji wake.

• Odhiambo tangu kustaafu kwake kutoka kandanda amekuwa akijihusisha katika biashara za uchukuzi wa umma.

Marehemu Mark Odhiambo
Marehemu Mark Odhiambo
Image: Facebook

Taarifa za Tanzia hivi punde ni kwamba aliyekuwa beki wa timu ya taifa ya Harambee Stars Mark Odhiambo ameaga dunia Jumanne asubuhi katika hospitali ya Coptic Mimmosa jijini Nairobi baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Kulingana na taarifa hizo za huzuni zilizochapishwa na wadau mbalimbali wa soka akiwemo mtangazaji wa Radio Jambo Fred Arocho, beki huyo ambaye alizichezea timu kadhaa za Kenya aliripotiwa kufariki mwendo wa saa tano asubuhi ya Jumanne Desemba 27 baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Odhimabo aliwahi zichezea timu za mpira wa miguu kama vile timu ya Mtaa wa Mbotela Kamaliza ambao ni mtaa mmoja mashariki mwa Nairobi alikokulia maisha yako ya utotoni, kabla ya kujiunga na timu ya vijana ya Mathare, Mathare United, Nakumatt FC mabingwa wa ligi ya KPL Tusker FC ambako alikuwa kama nahodha, Wazito FC miongoni mwa timu nyingine nyingi za humu nchini.

Mark alikuwa amestaafu soka na alikuwa katika biashara ya usafiri na uchukuzi wa abiria kwa matatu za umma, PSVs. Yeye ni mwanafunzi wa zamani wa St. Ignatius Mukumu Boys na pia alichezea timu ya taifa, Harambee Stars.

Kulingana na familia yake, alikuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kwa siku chache zilizopita baada ya kugundulika kuwa na uvimbe kwenye ubongo na kuganda kwa damu.