"Ni Uongo bana!" Rais wa Al Nassr akanusha tetesi za Ronaldo kujiunga na timu hiyo

Kwa wiki kadhaa majarida mengi yamekuwa yakiripoti kuwa Ronaldo amekubali mkataba na timu hiyo ya Al Nassr.

Muhtasari

• Rais Musli Al Muammar alisema kuwa nyingi ya tetesi kuhusisha klabu yake na Ronaldo ni uongo lakini pia hakufutilia mbali uwezekano wa klabu yake kuvizia huduma za staa huyo.

Al Nassr wakana kuhusishwa na Ronaldo
Al Nassr wakana kuhusishwa na Ronaldo
Image: Marca

Rais wa klabu wa Saudi Arabia ya Al Nassr kwa jina Musli Al Muammar amepuuzilia mbali taarifa ambazo zimekuwa zikichapishwa na majarida mbali mbali katika siku za hivi karibuni kuhusiana na uhamisho wa nyota wa Ureno Christiano Ronaldo kwenda klabuni humo.

Kulingana na rais huyo, taarifa hizo zinazomhusisha Ronaldo kukubali mkataba wa miaka 7, miwili kati yao ikiwa ni ya kuitumikia timu ya Al Nassr na mitano akiwa kama balozi wa timu hiyo ni uongo ambao umekuwa ukisambazwa na majarida ya bara Ulaya.

Ripoti hizo zilikuwa zimesema kuwa Ronaldo amekubali mkataba huo na alikuwa anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya akiwa Dubai na familia yake, na kuzama zaidi kuwa amekubali ofa ya dau pauni milioni 173 kwa mwaka, ofa ambayo ingemfanya kuwa mchezaji anayetia mfukoni kitika kikubwa zaidi.

Kulingana na jarida la The Sun, rais huyo wa Al Nassr alisema japo kuna baadhi ya madai na tetesi za ukweli, mengi ya madai ambayo yamekuwa yakichapishwa kuhusu Ronaldo kwenda klabu ya Al Nassr si kweli.

Aliiambia Flashscore:

"Siruhusiwi kusema ndio au hapana. Tusubiri tuone jinsi mambo yatakavyokuwa hadi mwisho wa mwaka. Kama unavyoona, haya ni mazungumzo ya ukubwa mkubwa, sio tu kwa klabu, lakini kwa nchi na soka ya dunia, na ambayo inapaswa kufanywa na mamlaka ya juu.”

Ronaldo mwenye umri wa miaka 37 aliondoka katika klabu ya Manchester United baada ya mkataba wake kusitishwa na timu hiyo kufuatia mahojiano makali aliyofanya na mwanahabari mtata Piers Morgan akitoa maneno ya nguoni dhidi ya klabu hiyo.

Kwa sasa ni mchezaji huru na anazidi kusaka klabu ya kuchezea, huku akiwa amehusishwa na timu kadhaa ndani na nje ya bara Uropa.