"Hautasahaulika na kumbukumbu yako itaishi milele" Ronaldo amuomboleza Pele

Pele alifariki Ahamisi Desemba 29 kutokana na saratani ya koloni akiwa na miaka 82.

Muhtasari

• Pele alifariki katika hospitali moja nchini Brazil akiwa na umri wa miaka 82 baada ya kupigana na saratani kwa muda mrefu.

• Ronaldo alimtaja kama kielelezo cha wengi katika malimwengu ya soka ambaye kumbukumbu yake haitakuja kusahaulika.

Ronaldo akiwa na Pele katika picha ya awali.
Ronaldo akiwa na Pele katika picha ya awali.
Image: Facebook

Alhamisi jioni taarifa za kifo cha aliyekuwa mshambuliaji hodari wa Brazil, Pele ziligubika ulimwengu mzima.

Pele alifariki katika hospitali moja nchini Brazil akiwa na umri wa miaka 82 baada ya kupigana na saratani kwa muda mrefu.

Watu mbalimbali wamemuomboleza mchezaji huyo aliyefana sana katika mashindano ya kombe la dunia kati ya mwaka 1958 hadi 1970 ambapo aliisaidia timu ya taifa ya Brazil kunyakua ubingwa wa dunia kwa mara tatu, mwaka 1958, 1962 na 1970 mtawalia.

Nyota wa Ureno Christiano Ronaldo amemuomboleza Pele na kumtaka kama baba yake katika malimwengu ya Soka ambaye alijifunza mengi kutokana naye hadi kukwea katika mafanikio yake.

Kupitia kurasa za mitandao ya kijamii, Ronaldo alipakia picha za zamani akiwa anapokezwa zawadi na Pele na kusema kuwa ni wakati mgumu sana kwa tasnia ya soka ulimwenguni kumpoteza nguli huyo zikiwa zimesalia siku mbili tu kuvuka mwaka.

“Alikuwa kielelezo kwa mamilioni mengi sana, kumbukumbu jana, leo na hata milele. Upendo ulionionyesha kila wakati ulirudiwa katika kila wakati tulioshiriki hata kutoka mbali. Hatasahaulika na kumbukumbu yake itaishi milele kwa kila mmoja wetu wapenzi wa soka. Pumzika kwa amani King Pele,” Ronaldo aliandika.

Hospitali ya Albert Einstein ya Sao Paulo, ambako Pele alikuwa akipatiwa matibabu, ilisema alifariki saa 3:27pm (18:27 GMT) siku ya Alhamisi "kutokana na kushindwa kwa viungo vingi kutokana na kuendelea kwa saratani ya koloni inayohusishwa na hali yake ya awali ya matibabu."