Rasmi! Ronaldo ajiunga na timu ya Al Nassr kutoka Saudia Arabia kwa dau nono ajabu

Ripoti nchini Saudi Arabia zinaeleza kuwa amesaini mkataba wa miaka miwili.

Muhtasari

• Inasemekana alimwaga wino kwa mkataba wa kuvutia wa pauni milioni 175 kwa mwaka.

• Mchezaji huyo amekuwa huru tangu kuachiwa na Manchester United kufuatia mahojiano ya kughadhabisha na mwanahabari mtata Piers Morgan.

Ronaldo akiwa pichani na rais wa Al Nassr
Ronaldo akiwa pichani na rais wa Al Nassr
Image: Insatgram

Klabu ya kandanda kutoka nchini Saudia Arabia Al Nassr hatimaye wamedhibitisha kuzinasa huduma za nyota wa Ureno Christiano Ronaldo.

Al Nassr walidhibitisha taarifa hizo kupitia ukurasa wao wa Instagram ambapo rais wa timu hiyo alionekana ameshika jezi pamoja na mchezaji Ronaldo na kusema kuwa kuzipata huduma zake ni zaidi ya historia ambayo klabu hiyo imeandikisha.

“Hii ni zaidi ya historia katika utengenezaji. Huu ni usajili ambao sio tu utaipa klabu yetu msukumo wa kupata mafanikio makubwa zaidi bali utaipa msukumo ligi yetu, taifa letu na vizazi vijavyo, wavulana na wasichana kuwa toleo bora zaidi lao. Karibu @cristiano kwenye familia yako mpya @alnassr_fc” Waliandika kwenye Instagram.

Ronaldo alithibitisha kuhamia kwa timu hiyo ya Saudi Arabia kwa mkataba wa kuvutia wa pauni milioni 175 kwa mwaka baada ya kuondoka kwa misukosuko kutoka Manchester United mwezi Novemba.

Ronaldo, mwenye umri wa miaka 37, alikuwa mchezaji huru baada ya kuondoka United baada ya mahojiano yake na Piers Morgan ambayo yalisumbua na ya kutatanisha, huku mashabiki sasa wakimiminika kwenye mitandao ya kijamii kudai kuwa 'ameisha' baada ya kuhamia Mashariki ya Kati.

Ripoti nchini Saudi Arabia zinaeleza kuwa amesaini mkataba wa miaka miwili.

Imedaiwa kuwa sehemu ya jukumu lake kama balozi ni kuisaidia Saudi Arabia katika ombi la pamoja na Misri na Ugiriki kuandaa Kombe la Dunia la 2030.

Anaungana na mpinzani wake mkuu Lionel Messi kuchukua nafasi ya upandishaji cheo na taifa hilo la Ghuba, ambalo limekabiliwa na ukosoaji kwa rekodi yake ya haki za binadamu, pamoja na kukandamizwa kwa wanaharakati wa haki za wanawake, LGBTQ+ na wale wanaozungumza dhidi ya utawala wa Mwanamfalme Mohammed bin Salman.