"Mzee ni wewe!" Arsene Wenger, 73, acheza densi kwa ustadi kukaribisha mwaka mpya (Video)

Wengi walimsifia kwa jinsi alivyokuwa akiinama na kuinuka bila taabu licha ya umri wake kuwa mkongwe.

Muhtasari

• Wengi walimsifia kwa jinsi alivyokuwa akiinama na kuinuka bila taabu licha ya umri wake kuwa mkongwe.

• Video hiyo ilipakiwa na Patrice Evra, aliyekuwa mchezaji wa Manchester United.

Aliyekuwa mchezaji wa zamani wa Manchester United Patrice Evra amewafurahisha mashabiki wengi wa soka baada ya kupakia video kocha mkongwe Arsene Wenger akicheza densi katika sherehe moja ya kufungua mwaka mpya 2023.

Katika klipu hiyo ambayo imewaunganisha mashabiki wa kandanda kote ulimwenguni, Wenger ambaye amevalia shati jeupe kama kawaida yake alionekana akikata kiuno kwa muziki akiwa na watu wengine ambao wote walikuwa na furaha ya ajabu kuukaribisha mwaka mpya.

Evra ambaye alipakia video hiyo alionesha furaha yake akisema kuwa bado mkongwe huyo alikuwa na nguvu na ustawi wa kufana kuhimili kucheza densi kwa tabasamu kubwa ikiwemo kuinama na kuinuka pasi na kupata taabu.

“Jumatatu njema @arsenal 🙏 arsene wenger sherehe ya kuaga mwaka na kukaribisha mwaka mpya ilikuwa ya ajabu 😳 ( wanasikiliza wimbo mmoja?” Evra aliandika mitandaoni.

Video hii inajiri siku chache tu baada ya kocha huyo aliyeinoa Arsenal kwa zaidi ya miaka 20 kuonekana kwa mara ya kwanza akiwa katika uwanja wa Emirates akifuatilia mechi ya Arsenal dhidi ya Westham, mechi ambayo wanabunduki waliibuka washindi na kuendeleza ubabe wao kileleni mwa jedwali.

Wenger alirejea Emirates kwa mara ya kwanza tangu alipoondoka mwaka 2018 baada ya kuhudumu kama kocha kwa miaia 22.

Wakati akihudumu kama mkufunzi mkuu wa timu hiyo, Arsenal ilishinda taji la ligi ya Premia mara tatu ikiwemo kushinda msimu wa mwaka 2003/04 bila kupoteza mechi hata moja.

Pia walishinda mataji 7 ya FA kipindi cha uongozi wa Wenger.