Chelsea wampe Potter muda, mimi sikuhitaji muda Barcelona, nilikuwa na Messi - Guardiola

Najua katika vilabu vikubwa, matokeo ni muhimu, lakini ningesema mpe muda - Guardiola.

Muhtasari

• Kocha huyo ambaye ameshinda mataji mengi na vilabu mbalimbali alimtetea mwenzake wa Chelsea akisema kuwa anahitaji muda ili kuijenga timu hiyo.

Guardiola amtetea Potter wa Chelsea kuwa anahitaji muda
Guardiola amtetea Potter wa Chelsea kuwa anahitaji muda
Image: Fabrizio Romano//Twitter

Mkufunzi mkuu wa timu ya Manchester City Pep Guardiola ameomba uongozi wa timu ya Chelsea kumpa muda kocha Muingereza Graham Potter na wala wasikurupuke kumwachisha kazi.

Akizungumza baada ya kukamilika kwa mecho ya FA iliyowakutanisha Chelsea na Manity usiku wa Jumapili ugani Etihad, Guardiola alizungumzia umuhimu wa muda katika kocha ambaye ametua kwenye timu mpya ambayo iko katika taratibu za kujenga kikosi cha mbeleni.

Kocha Potter anapitia wakati mgumu kama kocha wa Chelsea haswa baada ya kuwa na msururu wa matokeo mabaya tangu ligi kuu ya Premia kurejelea kutoka kwa likizo fupi ya mashindano ya kombe la dunia.

Chelsea ilikutana na City siku 3 zilizopita katika michuano ya EPL, mchezo ambao City waliibuka washindi kwa kuwanyuka Chelsea bao moja kappa na Jumapili tena wakarudia tukio hilo kwa kuwachabanga Chelsea mabao 4 kwa nunge katika mechi ya FA.

Baada ya Chelsea kupoteza, baadhi ya mashabiki walianza kupiga kelele za kumtaka kocha Potter kufutwa kazi lakini Guardiola alikuwa na ushauri tofauti kwa uongozi wa timu hiyo ambapo aliwataka kumpa muda kiasi kocha huyo.

Alipoulizwa mbona yeye hakuhitaji muda ili kujionesha katika klabu ya Barcelona miaka kadhaa iliyopita, Guardiola alisema kuwa kule ni tofauti kwa sababu alikuwa na mchezaji mmoja nguli kwa usakataji kabumbu duniani – Lionel Messi ambaye alimwezesha kufana katika msimu wake wa kwanza kama kocha.

“Ningemwambia Todd Boehly kwamba ilikuwa ni furaha kukutana naye, kwa hiyo mpe muda. Najua katika vilabu vikubwa, matokeo ni muhimu, lakini ningesema mpe muda. Katika Barcelona, ​​kulikuwa na sababu. Kwa sababu nilikuwa na Messi pale, sikuhitaji misimu miwili; msimu mmoja tu ulinitosha kung’ara sababu yake,” Guardiola alinukuliwa na jarida la Football London.

Chelsea sasa wanakalia nafasi ya kumi katika msimamo wa jedwali la ligi kuu ya EPL, wakiwa pointi 10 kutoka nafasi ya nne ambayo inawezesha timu kufuzu kombe la UEFA Champions League na pia pointi 10 kutoka eneo hatari la kushushwa dajala.