• FKF iiwarai viongozi na washikadau wa soka kote nchini kutojihusisha na masuala ya upangaji matokeo kabla ya shoka la marufuku halijatua utosini mwao.
Shirikisho la soka nchini Kenya FKF limewapiga marufuku baadhi ya wachezaji na wasimamizi wa michezo kufuatia skendo inayowahisisha na upangaji wa matokeo kwa kimombo ‘match fixing’
Katika barua ambayo ilitolewa na FKF Siku ya Ijumaa, wasimamizi wa michezo kadhaa pamoja na makumi ya wachezaji wataathirika kutokana na marufuku hiyo ambayo itaanza kufanya kazi mara moja.
Watu hao hawatoruhusiwa kwa njia yoyote ile kujihusisha na masuala ya kandanda mpaka pale uchunguzi dhidi yao utakapokamilika na huenda wakachukuliwa hatua kali za kisheria kulingana na taratibu na sheria za FIFA.
“Shirikisho la FKF limepokea taarifa za kinyemela zinazowahusisha baadhi ya wachezaji na wasimamizi wa soka katika sakata la upangaji matokeo. Katika juhudi za kulinda uadilifu wa ligi yetu, na kulingana na taratibu za shirikisho letu za kutokubali vitendo vyovyote vya upangaji matokeo, tumeamua kuwasimamisha wafuatao kutojihusisha na kandanda nchini,” sehemu ya barua ya FKF ilisoma.
Walipatwa na shoka hilo la FKF ni pamoja na Isaac Kipyegon wa Timu ya Tusker ambao ndio mabingwa watetezi wa KPL, Dennis Monda, mchezaji wa zamani wa Vihiga United, Willis Ochieng Oganyo ambaye ni kocha wa timu ya chuo cha Zetech miongoni mwa wengine.
Wengi wa waliopigwa marufuku ni kutoka timu ambayo imekuwa ikikumbwa na masaibu kwa miaka miwili iliyopita ya Zoo Kericho ambao wachezaji wake wengi walipatikana na hatia ya upangaji wa matokeo.
FKF iiwarai viongozi na washikadau wa soka kote nchini kutojihusisha na masuala ya upangaji matokeo kabla ya shoka la marufuku halijatua utosini mwao.