Kila kitu unafaa kujua kuhusu kadi nyeupe katika soka, kadi ya 3 baada ya nyekundu na njano!

Kadi hiyo ilitumiwa mara ya kwanza katika soka ya wanawake baina ya Benfica na Sporting Lisbon za Ureno.

Muhtasari

• Hii ni kadi ya 3 katika soka baada ya nyekundu na njano zilizoanzishwa mwaka wa 1970 katika mashindano ya kombe la dunia.

Kadi nyeupe katika mchezo wa soka
Kadi nyeupe katika mchezo wa soka
Image: Daily Mail// Screengrab

Wikendi iliyopita, historia iliandikishwa upya katika mechi ya kandanda nchini Ureno baada ya shirikisho la soka nchini humo kutambulisha kadi mpya nyeupe.

Mashabiki wamezoea kadi nyekundu na njano kwa faulo na makosa wakati wa mechi, ambayo ilitekelezwa zaidi ya miaka 50 iliyopita kwenye Kombe la Dunia la 1970.

Ureno sasa imeanzisha rangi ya tatu kama sehemu ya mfululizo wa mipango mipya nchini humo.

Kadi hiyo ambayo ni ya tatu sasa baada ya zile za rangi ya manjano na nyekundu ilitumiwa mara ya kwanza katika mechi ya wanawake baina ya timu za Sporting Lisbon a Benfica.

Lakini je, hii kadi nyeupe ni ya nini na dhima yake ni gani?

Kulingana na shirikisho la soka la Ureno, kadi hiyo inaweza kuonyeshwa ili kutambua na kuhimiza uchezaji wa haki na imeundwa 'kuboresha thamani ya kimaadili katika mchezo', jarida la Daily Mail liliripoti.

Hatua hiyo ni sehemu ya mpango mpya nchini Ureno wa kuhimiza pande zote kutenda kwa njia ya michezo na kupokea kutambuliwa papo hapo kwa matendo yao mazuri.

Kadi nyeupe hutoa utambuzi wa haraka kwa kitendo chanya wakati wa mechi ya kandanda. Kadi hii haitatolewa tu kwa wachezaji na waamuzi bali pia hata kwa matabibu wanapofanya kazi yao vyema uwanjani.

Mpango huo bado haujaenea na kwa sasa umetumwa kwa Ureno, lakini ni sehemu ya mfululizo mpana wa utambulisho mpya katika soka.

Itakumbukwa kuwa kadi nyeupe ilizungumziwa kwa mara ya kwanza mwaka 2014 na aliyekuwa rais wa shirikisho la soka barani ulaya UEFA Michel Platini lakini wazo lake halikutiliwa maanani sana.

Kulingana na Platini kipindi hicho, alitaka kadi hiyo kujumuishwa kwenye mchezo kama adhabu kwa wapinzani, ambayo ingewaacha wachezaji wenye hatia kwenye nje ya mchezo kwa angalau dakika 10.

Platini alipendekeza kadi hiyo nyeupe kusaidia kukabiliana na 'tamaa ya kugombea mwamuzi', ambayo aliitaja kama 'janga la kweli katika soka' – Jarida la Mirror lilisema.

Baada ya kadi hiyo kushuhudiwa kwa mara ya kwanza Ureno, sasa inasubiriwa kuonekana kama itatumika katika ligi zingine barani Ulaya au hata kuasisiwa katika mchezo wa soka kote duniani kama moja ya sheria za shirikisho la soka duniani FIFA.