AFC waiandikia FKF barua kutaka kuahirishwa kwa debi ya Mashemeji

Mechi hiyo baina ya AFC na Gor iliratibiwa kufanyika Januari 29 lakini Leopards wanaomba iahirishwe hadi Februari 5.

Muhtasari

• Walitaka FKF ikubali ombi lao kusongesha mechi hiyo hadi wikendi ijayo wakisema kuwa wadhamini wao walikuwa wameanza maandalizi ya Februari na si Januari.

Shirikisho la FKF limekataa kutoa kibali kwa AFC kupeperusha mechi yao na Police FC mitandaoni
Shirikisho la FKF limekataa kutoa kibali kwa AFC kupeperusha mechi yao na Police FC mitandaoni
Image: Facebook//AFC Leopards

Klabu ya AFC Leopards inayoshiriki ligi kuu ya Kenya KPL imeliandikikia shirikisho la soka FKF barua ya kutaka debi ya Mashemeji kati yao na mibabe Gor Mahia kuahirishwa.

Katika barua hiyo ambayo ilitiwa saini na mkurugenzi mkuu wa timu hiyo Victor Bwibo, Leopards walisema hawana uwezo wa kufika uwanjani kwa ajili ya mechi hiyo huku wakitaka ratiba yao na Gor kusukumwa mbele kiasi ili kutoa muda wa maandalizi.

Mashemeji Debi ilikuwa imeratibiwa kuchezwa wikendi hii ya Januari 29 lakini Leopards walionesha kusikitishwa kwao kuwa hio huenda halitawezekana na hivyo kutaka ratiba hiyo kusukumwa hadi Februari 5 kama walivyokuwa wameomba awali.

“Ikizingatiwa kwamba huu ni mchezo mkubwa wa kunadi sura ya shirikisho la FKF, maandalizi yake ni muhimu na ambayo yanahitaji mikakati kabambe. Isitoshe, tayari tuliuwa tumewaelewesha wadhamini wetu na washikadau kutoa usaidizi kwa maandalizi ya mechi yetu ambayo awali tulikuwa tumeweka akilini kuwa ingefanyika Februari 5. Mandalizi yalikuwa yameanza yakilengwa kwa tarehe hiyo. Tafadhali kubali ombi letu na samahani kwa mkanganyiko wowote ambao utakuwa umetokea,” sehemu ya barua hiyo ilisoma.

Wakati Leopards wanataka kuahirishwa kwa mechi, watani wao wa jadi Gor Mahia wanaendelea na maandalizi murua huku siku ya Alhamisi wakituma barua ya mwaliko rasmi kwa aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga ambaye ni shabiki sugu wa muda mrefu wa timu hiyo.

Katika barua yao, Gor pia walimuomba Odinga kuahirisha mkutano wake wa kisiasa unaotarajiwa kufanyika katika uwanja wa Jacaranda ili kupisha muda kwa debi hiyo kufanyika naye pia kupata kuhudhuria.