Harry Kane: Mshambuliaji mwenye rekodi nyingi nzuri bila medali

Usiku wa Jumapili, bao lake dhidi ya City lilimhakikishia nafasi katika chama cha wachezaji wenye mabao 200 na zaidi.

Muhtasari

• Desemba iliyopita, aliungana na Rooney kuwa wafungaji bora wenye mabao mengi - 53.

• Licha ya kuwa na taaluma yenye rekodi nzuri, Harry Kane hajawahi kushinda taji lolote la maana na timu ya Spurs wala Three Lions ya Uingereza.

Harry Kane, nahodha wa Spurs na Three Lions
Harry Kane, nahodha wa Spurs na Three Lions
Image: Facebook

Mchezaji wa timu ya Tottenham Hotspurs ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Uingereza Harry Kane amejinafasi kwenye vitabu vya historia ya soka baada ya bao lake la ushindi dhidi ya Manchester City usiku wa Jumapili.

Kwanza, Kane aliingia kwenye rekodi kama mchezaji wa Tottenham mwenye mabao mengi Zaidi katika historia ya klabu hiyo kwa mabao 267.

Bao lake lilivunjilia mbali rekodi na aliyekuwa mchezaji nguli wa klabu hiyo Jimmy Greaves aliyefunga mabao 266, rekodi ambayo imekuwa ikisimama tangu mwaka wa 1970.

Kando na kuweka rekodi mpya kwenye klabu, mchezaji huyo pia aliweka rekodi maridadi kwenye ligi kuu ya Uingereza kwa kuwa mchezaji wa tatu wa kufikisha mabao Zaidi ya 200.

Awali rekodi hiyo ilikuwa imeshikiliwa na wachezaji Allan Shearer, gwiji wa Newcastle aliyefunga mabao 260 akiitumikia Magpies na Wyne Rooney aliyefunga mabao 208 akizitumikia timu za Everton na Manchester United.

Kane aliweka rekodi kuwa mchezaji wa kufikisha mabao 200 akiwa ameshiriki mechi chache mno.

Shearer alifikisha mabao mia mbili baada ya kushiriki mechi 306, Rooney akifikisha mabao 200 baada ya mechi 462 huku Kane akivunja rekodi za wawili hao na kutinga mabao 200 baada ya alama 304.

Kimekuwa kipindi kisichosahaulika kwa Kane, ambaye alilingana na Rooney kama mfungaji bora wa pamoja wa England kwa mabao 53 alipofunga dhidi ya Ufaransa kwenye Kombe la Dunia mwezi Desemba.

Greaves, ambaye alifariki akiwa na umri wa miaka 81 mwaka 2021, anachukuliwa kuwa mmoja wa wafungaji wa asili zaidi katika historia ya soka. Akiwa katika kikosi cha England kilichoshinda Kombe la Dunia 1966, ambaye aliifungia nchi yake mabao 44, Greaves ndiye mfungaji bora zaidi katika historia ya Ligi Kuu England akiwa amefunga mabao 357.