Wachezaji wa kike wa Man U hawataki Mason Greenwood kurejeshwa timuni

“Wanahitaji kutoa taarifa sahihi na kumruhusu arudi litakuwa jambo baya zaidi wangeweza kufanya.”

Muhtasari

• Inaarifiwa kuwa baadhi ya wachezaji wa timu ya wanaume pia wanapinga uwezekano wa kurudishwa kwa Greenwood kwenye timu ya United.

• United alijipata kwenye sakata hilo mwaka mmoja uliopita baada ya mrembo wake kupakia picha za ukakasi akidai kuwa alishambuliwa naye.

Wanawake wa United hawamtaki Mason Greenwood.
Wanawake wa United hawamtaki Mason Greenwood.
Image: Twitter.

Siku chache baada ya mchezaji kinda wa Manchester United Mason Greenwood kufutiliwa mashtaka dhidi yake yaliyokuwa yakimkabili kwa madai ya kumshambulia na kumnyanyasa aliyekuwa mpenzi wake, bado kuna vizingiti vingi kabla yake kurejeshwa timuni.

Imebainika kwamba wachezaji wa timu ya wanawake ya Manchester United hawamtaki mchezaji huyo kurejeshwa kwenye timu wakisema kuwa rekodi yake ya kunyanyasa wanawake itawaathiri kisaikolojia.

Kulingana na Daily Mail, Maoni hayo yanachangiwa na timu ya wanaume, ambayo pia inadhaniwa kutofurahishwa na wazo la kurejea kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21, huku kikosi hicho kikihofia kuwa kinaweza kukwamisha maendeleo yao.

Greenwood kiufundi anaweza kuichezea United, kwani hajatangazwa kuwa na hatia au hana hatia ya mashtaka ambayo yalitupiliwa mbali.

Lakini bado haijafahamika iwapo mchezaji huyo atarejea katika timu ya Mashetani Wekundu, ikizingatiwa kwamba alisimamishwa tu na klabu mnamo Januari na malipo kamili.

Na tangu kufutwa kwa mashtaka hayo, Greenwood amehifadhi lebo za Manchester United kwenye ukurasa wake wa Instagram - pamoja na viungo vya mdhamini wake Nike ambaye alikatisha uhusiano wao na mchezaji huyo baada ya kukamatwa.

Mwanzilishi wa Klabu ya Wafuasi ya Wanawake ya Manchester United Natalie Burrell amezungumzia jinsi ambavyo hataki kumuona Greenwood akiwa na jezi nyekundu maarufu ya Manchester United tena.

Burrell pia alipendekeza kwamba kumruhusu fowadi huyo kurudi kwenye kundi kungetengua kazi iliyofanywa na mashirika ya misaada kama vile Her Game Too, ambayo inakuza ushiriki wa soka kwa wanawake.

"Sidhani kama anafaa kucheza tena Manchester United," Burrell aliambia jarida la Athletic. “Ni moja ya klabu kubwa duniani. Wanahitaji kutoa taarifa na kumruhusu arudi litakuwa jambo baya zaidi wangeweza kufanya.”

 

"Itarudisha klabu yetu nyuma katika suala la kile tunachojaribu kufanya na timu yetu ya wanawake na kampeni kama Her Game Too, ambazo zinajaribu kuhimiza wanawake kucheza na kutazama mpira wa miguu."