Pogba atoa ujumbe wa hisia baada ya kujeruhiwa tena, wiki moja baada ya kupona

"Mungu hampi mja wake mzigo asioweza kumtua," Pogba alijiliwaza baada ya kujeruhiwa tena wiki moja tu baada ya kupona jeraha la muda mrefu.

Muhtasari

• Kiungo huyo alicheza zaidi ya mechi 120 akiwa na Juventus kati ya 2012 na 2016, kabla ya kuhamia Manchester United.

• Hatimaye alirejea, lakini aliondolewa kwenye kikosi cha mechi ya Ligi ya Europa dhidi ya Freiburg wiki iliyopita kutokana na suala la kinidhamu

Pogba atoa ujumbe wa kihisia akirudi majeruhi tena.
Pogba atoa ujumbe wa kihisia akirudi majeruhi tena.
Image: Instagram

Wiki moja tu baada ya kupona jeraha la muda mrefu na kuruhusiwa kurejea uwanjani, mchezaji wa Juventus Mfaransa Paul Pogba tena amepata jeraha linguine ambalo litamweka nje ya uwanja kwa takriban wiki nne.

Tangu ajiunge tena na wababe hao wa Italia kutoka Manchester United Julai 2022, Pogba amekuwa akikabiliwa na majeraha - akishiriki mechi mbili pekee ambazo ni jumla ya dakika 35.

Sasa Juventus wamethibitisha kwamba Pogba mwenye umri wa miaka 29 'amepata jeraha la kiwango cha chini kwenye paja lake la kulia', na ameanza mchakato wa ukarabati kwa nia ya kurejea katika hatua ya kiushindani.

Mchezaji huyo alirejea uwanjani wiki moja iliyopita lakini akafungiwa kushiriki mechi kufuatia adhabu aliyopewa baada ya kufika kwenye mazoezi akiwa amechelewa.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Pogba aliachia ujumbe wa kihisia akisema kwamba anaamini kila kitu hutokea kwa sababu kutoka kwa Mungu na kwamba Mungu hawezi akampa mtu mtihani ambao hawezi kuumudu.

“Mungu hawezi kumpa mja wake mzito mzito ambao hawezi kumudu kuubeba,” Pogba aliandika.

Kiungo huyo alicheza zaidi ya mechi 120 akiwa na Juventus kati ya 2012 na 2016, kabla ya kuhamia Manchester United.

Pogba alirejea Juventus majira ya kiangazi mwaka jana kwa mkataba wa miaka minne kwa mkataba unaomletea kitita cha pauni milioni 8.8 kila baada ya miezi 12, lakini amekuwa na matatizo ya kuwa fiti baada ya kurejea.

Kujeruhiwa kwa goti wiki mbili baada ya kujiunga kulimaanisha kwamba mwanzo wake ulichelewa, na Mfaransa huyo baadaye alihitaji upasuaji ambao ulimtoa nje ya Kombe la Dunia.

Hatimaye alirejea, lakini aliondolewa kwenye kikosi cha mechi ya Ligi ya Europa dhidi ya Freiburg wiki iliyopita kutokana na suala la kinidhamu baada ya kuchelewa kufika kwenye kikao cha timu. Pogba aliutazama ushindi wa 1-0 kutoka kwa viti.