Babake Ansu Fati amemsakama koo kocha wa Barcelona kwa kutomchezesha mtoto wake

"Wakati akiwa na majeraha, walimlazimisha kucheza ili kufurahisha mashabiki, lakini sasa yuko fiti 100%, hapewi nafasi ya kucheza, mbona?"

Muhtasari

• Fati amevumilia majeruhi ya mara kwa mara, lakini baada ya kuyashinda, tangu wakati huo alipata muda mchache wa kucheza chini ya bosi Xavi.

• Jambo la kuingizwa mchezo kwa dakika chache limemkera babake ambaye sasa anamshauri kinda huyo kuondoka Barcelona.

Babake Ansu Fati ataka majibu kwa nini Fati hachezi
Babake Ansu Fati ataka majibu kwa nini Fati hachezi
Image: Inatagram

Babake Ansu Fati, Bori, amefichua kuwa amemtaka mwanawe kuondoka Barcelona iwapo muda wake wa kucheza hautaimarika.

Bori, katika mahojiano ya kipekee mapema Jumatano alitoa cheche kali dhidi ya klabu ya Barcelona na haswa kocha Xavi kwa kumkalisha mwanawe kwenye benchi licha ya kuwa fiti kwa asilimia 100.

Mhitimu huyo wa La Masia alijitokeza uwanjani akiwa na umri wa miaka 16, na kurithi jezi nambari 10 wakati Lionel Messi alipoondoka kwenda Paris-Saint Germain majira ya joto ya 2021.

Fati amevumilia majeruhi ya mara kwa mara, lakini baada ya kuyashinda, tangu wakati huo alipata muda mchache wa kucheza chini ya bosi Xavi.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 ameanza mechi tisa pekee hadi sasa msimu huu, na kushiriki mara 15 kwa vinara hao wa LaLiga akiingizwa kama nguvu mpya.

Babake Bori amefichulia kwa kituo cha redio cha Uhispania Cope kuwa amekasirishwa na hali hiyo, akimshauri mwanawe kuondoka Camp Nou.

“Wakiwa Barca wananiambia kuwa wameweka dau sana juu ya Ansu, wananiambia hivyo waziwazi," Bori Fati alisema.

“Nilipokaa na Jorge Mendes, jambo la kwanza aliniambia ni kwamba Ansu anataka kubaki na ataendelea kuichezea Barcelona. Lakini mimi, kama baba, nilifikiria vinginevyo, na Ansu hakubaliani na hilo. Kinachonisumbua ni jinsi wanavyomchukulia Ansu kwa dakika. Dakika moja, dakika mbili, dakika tatu, hiyo ndiyo inanisumbua."

"Barca ilipokuwa mbovu zaidi kuliko ilivyo sasa, walimlazimisha Ansu Fati kurejea kutoka kwenye majeraha ili kucheza. Walikuwa wakimtaka Ansu awafurahishe tena watu. Kwasasa yuko fiti 100% na yuko tayari, hakuna anayemtaka Ansu?"

Mkutano unatarajiwa kufanyika kwa wakati ufaao kati ya babake Ansu, Ansu mwenyewe na wakala Jorge Mendes kuhusu mustakabali wa vijana.

Fati, ambaye yuko chini ya mkataba na Barcelona hadi msimu wa joto wa 2027, hana mpango wa kuondoka makao ya wababe hao wa Catalan, huku wakuu wa Barca Jordi Cruyff na Mateu Alemany wakisisitiza kuwa yeye ni sehemu yao.

Manchester United, Arsenal na Liverpool zote zimewahi kuhusishwa na kijana huyo mwenye kipaji cha kipekee.