Mchezaji na Kocha wa zamani wa Chelsea Frank Lampard arudi Stamford Bridge

Kufikia sasa Chelsea haina kocha baada ya Potter kufutwa wikendi iliyopita. Mashabiki wanahisi kurejea kwake ni kama anataka kuchukua wadhifa huo.

Muhtasari

• Lamard alikuwa mchezaji wa zaidi ya miaka 15 ya timu hiyo kabla ya kuteuliwa kama kocha tena.

• Lakini mwaka 2021, kocha huyo alifutwa kazi baada ya Chelsea kuwa na mwendelezo wa matokeo duni.

Lampard aonekana Stamford Bridge
Lampard aonekana Stamford Bridge
Image: Twitter

Usiku wa Jumanne kulikuwa na mechi kubwa katika ligi kuu ya Premia kati ya Chelsea na Liverpool, timu ambazo zimekuwa na msimu mbaya na kufikia sasa zote ziko nje ya nne bora kushiriki ligi ya mabingwa msimu kesho.

Katika mechi hiyo ambayo ilichezewa uga wa nyumbani wa Chelsea, Stamford Bridge, mchezaji na kocha wa zamani Frank Lampard ni mmoja wa watu wengi waliojitokeza kushuhudia kipute hicho.

Ikumbukwe mpaka sasa Lampard hana kazi baada ya kutimuliwa Everton miezi miwili iliyopita kufuatia msururu wa matokeo mabaya wa timu hiyo majirani wa Liverpool.

Vile vile, Chelsea mpaka sasa hawana kocha baada ya kutimuliwa kwa Graham Potter wikendi iliyopita kufuatia kipigo cha mabao mawili kwa sifuri nyumbani dhidi ya Aston Villa.

Chelsea waliongozwa na kocha msaidizi Bruno Saltor katika sare kapa dhidi ya Liverpool na kuonekana kwa Lampard timuni humo kuliwaacha mashabiki wakizungumza kuwa huenda pia ni mmoja wa wale wanaoweza kuchukua nafasi ya ukocha.

Hii ndio mara ya kwanza kwa Muingereza huyo kuonekana Stamford Bridge tangu kufutwa kazi mwaka 2021.

“Huyu ndiye mbadala wa Potter?” baadhi ya mashabiki waliuliza kwenye mtandao wa Twitter.

“Kukutana tena kwa mara ya tatu huko Stamford Bridge? Chelsea wanadaiwa kufikiria kumrudisha Frank Lampard kama kocha wa muda hadi mwisho wa msimu huu!” mwingine aliibua madai.

Hata hivyo, majarida mbalimbali yamekuwa yakiripoti tangu wikendi kuwa timu hiyo imewafikia aliyekuwa kocha wa Uhispania Luis Enrique na aliyekuwa kocha wa Bayern Munich Julian Nagelsmann kama mbadala wa Potter.