Kwa nini Lukaku alionyeshwa kadi nyekundu licha ya kubaguliwa kwa rangi ya ngozi

Mchezaji huyo baada ya kubaguliwa na mashabiki, alifunga bao na kusherehekea akiwanyamazisha kwa ishara ya kidole mdomoni.

Muhtasari

• Mechi ya Juventus na Inter Milan iliishia sare ya bao moja na Lukaku alikuwa mkombozi dakika ya 95.

• Kulingana na mwamuzi, mchezaji huyo alisherehekea mbele ya mashabiki wa timu pinzani akichochea hasira zao.

Romelu Lukaku aonyeshwa kadi nyekundu baada ya kufunga bao na kuwanyamazisha mashabiki wa timu pinzani.
Romelu Lukaku aonyeshwa kadi nyekundu baada ya kufunga bao na kuwanyamazisha mashabiki wa timu pinzani.
Image: Facebook//Chelsea

Jumanne usiku, nchini Italia kuliuwa na mechi kubwa baina ya mibabe Inter Milan na Juventus, mechi ambayo iliishira kwa sare ya bao moja moja.

Lakini kitendo kisichi cha kawaida kilishuhudiwa baada ya mashabiki wa Juventus kumtukana kwa kumbagua kwa rangi ya ngozi yake mshambuliaji wa Chelsea aliyeko mkoponi Inter Milan, Romelu Lukaku.

Lukaku, raia wa Ubelgiji mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alikuwa gumzo kubwa baada ya kubaguliwa waziwazi na mashabiki wa Juventus, jambo ambalo lilizua ukakasi mkubwa kwenye mechi hiyo ambayo ilikuwa na uzito wa aina yake.

Hata hivyo, mambo yalichukua mkondo tofauti kunako dakika ya 95 wakati Lukaku ambaye alikuwa amebaguliwa kufunga bao la kusawazisha na kukimbia kusherehekea mbele ya mashabiki wa Juventus kama njia moja ya kulipa kisasi kwa ubaguzi wa rangi.

Refa wa mchezo huo badala yake alimuonesha Lukaku kadi nyekundu kwa kuchochea mashabiki wa timu pinzani na kumtuma nje ya uwanja.

Lakini kitendo cha mashabiki hao kumbagua kwa rangi ya ngozi Lukaku kimezua mjadala mkali mitandaoni, wengi wa wapenzi wa mchezo wa soka wakikosoa mashabiki wa Juventus.

Aliyekuwa mshambuliaji wa Chelsea na timu ya taifa ya Ivory Coast Didier Drogba ametoa tamko kali dhidi ya kitendo hicho akisema kuwa ni ujinga uliopitiliza.

“Kipaji chako na nguvu zako zinapoanza kuwaumiza na unakuwa mkubwa na bora zaidi, ujinga wao hutokea 💪🏿 @romelulukaku,” Drogba alisema akimpa moyo Lukaku kuwa asinyamazishwe na masimango uwanjani.

Jumatano vile vile timu yake ya Chelsea ilitoa tamko sawa na hilo kupitia kurasa zao mitandaoni, ikisema kuwa inasimama na Lukaku kipindi hiki ambapo amebaguliwa kwa rangi ya ngozi yake.

“Tuko na wewe Lukaku,” Chelsea waliandika.

Mshambulizi huyo wa Ubelgiji alisherehekea kwa kuweka kidole chake mbele ya mdomo wake, pia akisema "nyamaza" kwa mashabiki wa nyumbani waliomlenga tangu alipoingia uwanjani kipindi cha pili.

Sheria inasema kwamba mchezaji lazima apewe kadi ikiwa atawaudhi mashabiki wanaompinga, hata hivyo, katika kesi hii, uamuzi wa mwamuzi unaonekana kuwa mkali, ikizingatiwa kuwa mshambuliaji tayari alisherehekea kwa njia ile ile nyakati zingine hapo awali na aliepuka kuonyeshwa kadi, CBS waliripoti.

 Haijulikani kuhusu afisa wa mechi hiyo alisikia dhuluma hiyo ya rangi lakini alibainisha baada ya mechi kuwa nafasi hiyo ilikuwa ya "kusherehekea kupita kiasi.”