Pigo kwa Wanabunduki huku Arteta athibitisha William Saliba kukosa mechi zaidi

Mashabiki wengi wamekuwa wakisubiri kwa hamu kurejea kwa Saliba wakitumai kutaboresha matokeo.

Muhtasari

•Arteta alitangaza kuwa kupona kwa beki huyo mwenye umri wa miaka 22 kunachukua muda zaidi kuliko ilivyotarajiwa.

•Arteta alidokeza kwamba beki huyo mahiri anafanya shughuli kadhaa nje ya uwanja za kumsaidia kupona kikamilifu.

William Saliba aongozwa nje baada ya kujeruhiwa.
Image: HISANI

Beki wa kati mahiri wa Arsenal, William Saliba anatarajiwa kukosa kucheza mechi kadhaa zaidi  huku akiendelea na matibabu.

Wakati wa kikao na wanahabari kabla ya mechi yao ya Ijumaa dhidi ya Southampton, kocha Mikel Arteta alitangaza kuwa kupona kwa beki huyo mwenye umri wa miaka 22 kunachukua muda zaidi kuliko ilivyotarajiwa.

Arteta alidokeza kuwa mchezaji huyo ambaye hajacheza kwa takriban mwezi mmoja tangu apate jeraha la mgongo wakati wa mechi ya Ligi ya Europa na klabu ya Sporting Lisbon ya Ureno atarejea kwenye mazoezi kamili wakato watakapokuwa na uhakika kuwa yuko tayari kurejea uwanjani.

"Haendelei haraka kama tulivyotarajia na ni dhaifu kwa hivyo tunataka kuwa na uhakika kuwa tunapomsukuma, yuko tayari kuchukua mzigo na hatari ambayo tutachukua, na hilo haliwezekani kwa sasa," Arteta alisema.

Aliposukumwa kujibu kuhusu ikiwa mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Ufaranza atakuwepo kwa mechi yoyote kati ya saba za mwisho, Mikel aliongeza: "Sijui, ni mapema kujua. Pengine wiki ijayo tutakuwa na uhakika zaidi."

Kocha huyo alidokeza kwamba beki huyo mahiri anafanya shughuli kadhaa nje ya uwanja za kumsaidia kupona kikamilifu.

Kutokuwepo kwa Saliba kunamaanisha Rob Holding atakuwa kwenye mstari wa kuanza tena na Arteta alikuwa mwepesi wa kumsifu pamoja na Kieran Tierney ambaye wikendi alicheza nafasi ya beki mwingine aliyejeruhiwa, Oleksandr Zinchenko.

"Kwanza kabisa jinsi wanavyofanya kwenye timu, jinsi wamekuwa wavumilivu, na wanapopaswa kucheza, kile ambacho wamefanya ni bora," alisema.

Wanabunduki wamekosa ushindi katika mechi mbili za EPL ambazo zimepita na idadi kubwa ya mashabiki imelaumu safu ya ulinzi. Mashabiki wengi wamekuwa wakisubiri kwa hamu kurejea kwa Saliba wakitumai kutaboresha matokeo.