‘Taji lipo mikononi mwetu’ Guardiola asema baada ya Manchester City kuizaba Arsenal mabao 4-1

City wamebakisha mechi saba, wakianza na safari ya Jumapili dhidi ya Fulham na mechi za nyumbani dhidi ya West Ham na Leeds.

Muhtasari

• Kikosi cha Pep Guardiola, sasa kiko pointi mbili nyuma ya Arsenal kikiwa na michezo miwili mkononi.

Image: BBC

Pep Guardiola anasema kuwa kikosi chake cha Manchester City kimethibitisha kuwa kinaweza kufanya kazi wakati hakuna "chaguo zaidi ila kushinda" baada ya kuishinda Arsenal na kuweka mikononi mwao kinyang’anyiro cha kushinda ubingwa wa Ligi ya Premia .

Kikosi cha Guardiola kiliwashinda viongozi Arsenal 4-1 kwenye Uwanja wa Etihad, na sasa wako nyuma kwa pointi mbili wakiwa na michezo miwili ya ziada .

City wamebakisha mechi saba, wakianza na safari ya Jumapili dhidi ya Fulham kabla ya mechi za nyumbani dhidi ya West Ham na Leeds.

"Hatuwezi kupoteza umakini wetu. Sasa iko mikononi mwetu," alisema Guardiola.

Manchester City walifanya vyema na kuwalemea viongozi wa Ligi ya Premia Arsenal na kuwapa pigo kubwa la kisaikolojia katika jitihada za kushinda ubingwa wa ligi huko Etihad .

Makabiliano hayo yaliyodaiwa kuwa mwamuzi wa taji yaligeuka na kuwa jambo la aibu kwa upande mmoja.

Kikosi cha Pep Guardiola, sasa kiko pointi mbili nyuma ya Arsenal kikiwa na michezo miwili mkononi, kilichochewa na ushirikiano hatari wa Erling Haaland na Kevin de Bruyne.

City wanaweza kwenda kileleni kwa ushindi dhidi ya Fulham siku ya Jumapili huku Arsenal wakilazimika kwa namna fulani kujiondoa kwenye mdororo ambao umewafanya kucheza mechi nne za ligi bila kushinda katika hatua muhimu ya msimu huu.