Mara ya mwisho timu ilishinda EPL mara 3 kwa mpigo, msimu uliofutata Chelsea walishinda...

Baadhi ya wachanganuzi wakirejelea historia ya nyuma, wanahisi baada ya City kuweka rekodi sawa na United kushinda EPL mara tatu kwa mfululizo, Chelsea watashinda mwaka 2024.

Muhtasari

• Chelsea walishinda EPL mwaka 2010 baada ya United kushinda mara tatu kwa mpigo kati ya mwaka 2006 hadi 2009.

• Wengi wanahisi Chelsea itarudia rekodi hiyo mwaka 2024 baada ya City kushinda kati ya mwaka 2021 hadi 2023.

Wengi wanahisi Cheslea itarejelea historia ya 2010 kushinda ligi baada ya mpinzani kuishinda mara 3 kwa mfululizo.
Wengi wanahisi Cheslea itarejelea historia ya 2010 kushinda ligi baada ya mpinzani kuishinda mara 3 kwa mfululizo.
Image: GOAL//Twitter.

Kama wewe ni mtu wa kuamini katika matukio ya kifikirika tu, basi hili pia litakupata sawasawa, na haswa ikitokea wewe ni shabiki wa Chelsea basi utakuwa na kila sababu ya kufurahi.

Wiki jana baada ya timu ya Manchester City kutawazwa mabingwa wa ligi kuu ya Premia nchini Uingereza, ulikuwa ni ubingwa wao wa tatu kwa kufuatana, na hilo limeibua tetesi kali za takwimu za misimu ya nyuma ambayo inaashiria na kuiweka Chelsea katika nafasi nzuri ya kuwa mabingwa msimu ujao wa 2023/2024.

Mitandaoni kwa muda wa wiki moja sasa, wadadisi na wachanganusi wa historia ya soka nchini Uingereza wameibua matukio ambayo yanaunga mkono kwa asilimia kubwa uwezekano wa Chelsea kushinda EPL msimu uliofuata.

Kwa mfano, baadhi ya wachanganuzi hao walirudisha muda nyuma na kuangalia kipindi ambapo kocha mstaafu Sir Alex Ferguson aliongoza Manchester United kushinda ubingwa wa EPL mara tatu kwa mfululizo kutoka mwaka wa 2006 hadi mwaka wa 2009, na mwaka uliofuata wa 2010 Chelsea walishinda ligi ya premia wakiwa na kocha Muitaliano, Carlo Ancelotti.

Kwa kigezo hiki, wengi wanahisi kwamba baada ya Mhispania Pep Guardiola kuisaidia Manchester City kushinda EPL kwa mara tatu mfululizo kati ya mwaka 2021 hadi 2023, huenda kocha ajaye wa Chelsea, Muargentina Mauricio Pouchettino akaisaidia timu hiyo kushinda ubingwa mwaka kesho.

“Mara ya mwisho timu ya EPL ilishinda ubingwa wa premia mara tatu kwa mpigo, msimu uliofuata Chelsea walishinda…” mmoja wa wachanganuzi alianzisha mjadala Twitter.

Hata hivyo, wengine pia walimuunga mkono kwa kuibua takwimu zingine za hivi karibuni msimu wa 2015/16 wakati malimbukeni Leicester City walipowashangaza wengi kwa kushinda EPL kukiwa na mechi chache kuelekea mwisho wa msimu, mechi iliyofuata ilikuwa dhidi ya Chelsea ambapo Chelsea walilazimika kuwaundia gwaride la heshima mabingwa hao na msimu uliofuata Chelsea wakaibuka mabingwa.

Tukio sawia na hilo limeshuhudiwa juzi baada ya City kuibuka mabingwa, mechi iliyofuata walicheza dhidi ya Chelsea na miamba hao wa London waliunda gwaride la heshima kwa City.