SOKA KIMATAIFA

Kwa nini Kombe la FA litaelekezwa Manchester United Wikendi

Tangu washinde EPL mchezo wao umedorora kwa kiasi kikubwa

Muhtasari

•Pep amepata sare na kupoteza mara moja katika mechi zake mbili za mwisho.

•Manchester United imepata ushindi katika mechi zao nne za mwisho,jambo ambalo limewapa motisha katika kinyang’anyiro hicho cha kombe la FA.

Wikendi ijayo Juni 3 kutakuwa na ngarambe ya kufa kupona katika mashemeji wa vilabu vya Manchester.

Man City baada ya kuibandua Sheffield United mwezi Aprili kwa mabao 3-0 watakuwa wakikabana koo na jirani wao United ambayo iliponea mikononi mwa Brighton katika mikwaju ya penati 7-6.

Vilabu vyote viwili vimekuwa na mchezo wa kufana zaidi katika ligi ya Primia ambayo ilifikia tamati wikendi iliyopita, ambapo Pep Guadiola alipata afueni tangu wapinzani wao wa karibu Arsenal walipopoteza mechi yao iliyokuwa ya kubaini bingwa dhidi ya Nottingham Forest.

Zipo sababu ambazo kuna uwezekano mkubwa vijana wa Erik Ten Hag wataipiku City katika fainali inayosubiriwa  katika fainali ya kombe la FA.

Manchester United imepata ushindi katika mechi zao nne za mwisho,jambo ambalo limewapa motisha katika kinyang’anyiro hicho cha kombe la FA. Pia klabu ya Ten Hag imemaliza ligi ikiwa katika nafasi nzuri kushindana katika ligi ya mabingwa msimu ujao. Kando na hayo, timu hiyo mapema mwaka wa 2023 alivikwa taji la Carabao lililowapa hamu zaidi kwenye ligi kuu Uingereza.

Kwa upande wake City, tangu watangazwe mabingwa wamekuwa wakizuazua katika mechi zilizokuwa zimesalia, ingawa waliudhabiti ubingwa wao kwa kuifunga Chelsea,tangu hapo hawajakuwa na mchezo wenye kuridhisha sana kama United. Pep amepata sare na kupoteza mara moja katika mechi zake mbili za mwisho kile ambacho kimechochea City kupunguza alama tano.

Licha ya hayo,Guardiola alieleza kuhusu uchovu uliowapata vijana wake jambo ambalo lilimfanya kutumia wachezaji wengi wa akiba kama waanzilishi katika mechi zao tatu za mwisho. Pia, alieleza sherehe za unywaji pombe walizokuwa nazo katika mji wa Manchester hivi kwamba ukinaifu iliwakaba vijana hao. Iwapo atawachezesha wachezaji hao waliotangulia katika mechi tatu za awali, hali ya Manchester ambao kwa sasa wapo katika mfumo mzuri bila shaka kuna uwezekano wao kutwikwa taji hilo la FA.

Manchester City pia  inapania kulinyakua taji la ligi ya mabingwa maarufu UEFA kwa mara ya kwanza, watakapokuwa wakimenyana na Inter Milan Juni 10. Iwapo watayanyakua mataji yote matatu msimu huu, ni jambo linalosubiriwa katika mechi yao dhidi ya United.