Eden Hazard hatimaye atemwa na Real Madrid baada ya misimu 4 ya mchezo hafifu

Hazard hatakuwa tena mchezaji wa klabu ya Real Madrid kuanzia mwisho wa Juni 2023.

Muhtasari

•Katika taarifa ya Jumamosi, Real Madrid ilitangaza kwamba Hazard na klabu hiyo wamefikia makubaliano ya kusitisha mkataba wake.

•Hazard alikuwa mchezaji anayelipwa zaidi Madrid kwa umbali fulani, akiripotiwa kuchumai zaidi ya pauni 500,000 kwa wiki.

hatakuwa mchezaji wa Real Madrid kuanzia mwisho wa Juni.
Eden Hazard hatakuwa mchezaji wa Real Madrid kuanzia mwisho wa Juni.
Image: HISANI

Mchezaji wa Kimataifa wa Ubelgiji Eden Hazard hatakuwa tena mchezaji wa klabu ya Real Madrid kuanzia mwisho wa Juni 2023.

Katika taarifa ya Jumamosi, Real Madrid ilitangaza kwamba Hazard na klabu hiyo wamefikia makubaliano ya kusitisha mkataba wake.

"Klabu ya soka ya Real Madrid na Eden Hazard wamefikia makubaliano ambapo mchezaji huyo ataondoka katika klabu hiyo kuanzia tarehe 30 Juni 2023," taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti rasmi ya Real Madrid ilisomeka.

Iliendelea,"Eden Hazard amekuwa sehemu ya klabu yetu kwa misimu minne, ambapo ameshinda mataji 8: Kombe 1  la Uropa, Kombe 1 la Dunia la Klabu, Kombe 1 la Uropa, Mataji 2 ya LaLiga, Copa del Rey 1 na Super Cups 2 ya Uhispania."

Staa huyo wa zamani wa Chelsea mwenye umri wa miaka 32 alijiunga na Real Madrid mwaka 2019 na mkataba wake uliratibiwa kumalizika mwaka ujao. Mchezo wake katika klabu hiyo ya Uhispania katika miaka minne iliyopita  hata hivyo haujatimiza matarajio ya mashabiki wengi wa soka ikizingatiwa fomu nzuri ambayo alikuwa nayo  wakati akinunuliwa kutoka The Blues kwa pauni milioni 86.

"Real Madrid ingependa kuonyesha upendo wetu kwa Eden Hazard na tunamtakia yeye na familia yake kila la heri katika hatua inayofuata ya maisha yake ya soka," Real ilisema huku ikimuaga mchezaji huyo wa kimataifa wa Ubelgiji.

Hazard amehusishwa mara chache sana kwenye mechi za Real Madrid katika msimu ambao umetamatika wa 2022/23 kutokana na kiwango hafifu cha mchezo wake. Wachezaji wadogo walio na uzoefu mdogo kuliko yeye wamependekezwa kucheza katika nafasi yake katika mechi nyingi za klabu hiyo.

Imeripotiwa kwamba Real imekuwa ikijaribu kumfukuza Hazard kwa muda, lakini mchezaji huyo amekuwa akisisitiza mara kwa mara kwamba anataka kubaki.

Hazard alikuwa mchezaji anayelipwa zaidi Madrid kwa umbali fulani, akiripotiwa kuchumai zaidi ya pauni 500,000 kwa wiki.