Inter Miami yapata wafuasi zaidi ya milioni 3.2 baada ya Messi kutangaza kujiunga nao

Kabla ya tangazo hilo kutoka kwa Messi, Klabu hiyo inayoshirikia ligi ya MLS nchini Marekani ilikuwa na wafuasi milioni moja peke yake.

Muhtasari

• Mchezaji alidhibitisha uvumi uliokuwa ukienea kuhusu uhamisho wake na kusema kuwa sasa chaguo lake ni kujiunga na timu ya Inter Miami.

• Mshindi huyo wa kombe la dunia alifutilia mbali ripoti zilizokuwa zikienezwa kuhusu kurejea kwake kwa timu yake ya zamani ya Barcelona.

• Lionel Messi alikataa kujiunga na timu ya Al-Hilal baada ya timu hiyo kuutaka kujiunga no kwa mkataba ukatao wagharimu  dola bilioni moja (Shilingi bilioni 139.15 za Kenya).

Image: INSTAGRAM// LIONEL MESSI

Timu ya Inter Miami imepata wafuasi wapya milioni 3.2 katika akaunti yake ya Instagram baada ya mchezaji Lionel Messi kutangaza kujiunga na timu hiyo.

Kabla ya tangazo hilo kutoka kwa Messi, Klabu hiyo inayoshirikia ligi ya MLS nchini Marekani ilikuwa na wafuasi milioni moja peke yake.

Ndani ya saa moja baada ya mwanahabari tajika wa maswala ya uhamisho ya wachezaji wa soka, Fabrizio Romano kuzungumzia chaguo la Messi kuhamia klabu hiyo, klabu hiyo ilipata wafuasi zaidi ya milioni moja na kuongeza wafuasi katika akaunti hiyo maradufu. 

Mchezaji huyo ambaye alitangaza kuondoka kwake PSG baada ya msimu huu wa 2022/2023 kukamilika, alidhibitisha uvumi uliokuwa ukienea kuhusu uhamisho wake na kusema kuwa sasa chaguo lake ni kujiunga na timu ya Inter Miami.

Akizungumza Jumatano kuhusu tetesi zilizoenea katika mitandao ya kijamii kuhusiana na uhamisho wake, Messi alisema kuwa ameichagua timu hiyo inayomilikiwa na mchezaji wa zamani wa Manchester United David Beckham.

"Chaguo langu ni kuenda timu ya Inter Miami na siendi huko kwa sababu ya pesa kwa kuwa kama ni kwa sababu ya hela ningejiunga na timu ya Al-Hilal inayoshiriki ligi ya Saudi Arabia kwa sababu huko ningepata pesa nyingi kuliko Marekani" Messi alisema.

Mshindi huyo wa kombe la dunia alipuuzilia mbali ripoti zilizokuwa zikienezwa kuhusu kurejea kwake kwa timu yake ya zamani ya Barcelona na kusisitiza kuwa hakutaka kupitia kile alichopitia kabla ya kulazimika kujiunga na timu ya PSG katika dirisha la uhamisho wa msimu wa joto wa mwaka wa 2021.

"Nilipendelea kujiunga na Barcelona, nilikuwa na ndoto hiyo kwa muda mrefu sasa. Lakini baada ya kile kilichotokea miaka miwili iliyopita, sikutaka kuwa katika hali kama hiyo tena, kuacha maisha yangu ya baadaye kuamuliwa na mtu mwingine."