Jorginho amkaribisha rasmi aliyekuwa mchezaji mwenzake, Kai Havertz katika Arsenal

Arsenal imekamilisha usajili wa winga Kai Havertz kutoka Chelsea kwa takriban pauni milioni 65.

Muhtasari

•Jorginho alichapisha picha yake akibarizi na Havertz na kuambatanisha na vidokezo kwamba winga huyo mwenye umri wa miaka 24 hivi karibuni atakuwa mchezaji mwenzake tena.

•Havertz anahamia Emirates miezi michache tu baada ya Jorginho kukamilisha uhamisho wake kwa dau la pauni milioni 12. (Ksh 2.1 bilioni).

Kai Havertz akifurahia muda na Jorginho
Image: HISANI

Kiungo wa kati wa Arsenal Jorginho Frello ameonekana kuthibitisha kuwa mchezaji mwenzake wa zamani katika klabu ya Chelsea, Kai Havertz yuko karibu sana kujiunga naye katika upande wa kaskazini mwa London.

Siku ya Jumamosi, mchezaji huyo wa kimataifa wa Italia alichapisha picha yake akibarizi na Havertz na kuambatanisha na vidokezo kwamba winga huyo mwenye umri wa miaka 24 hivi karibuni atakuwa mchezaji mwenzake tena.

Wawili hao walikutana na kushiriki wakati mzuri kwenye harusi ya mlinda lango wa The Blues, Kepa Arrizabalaga siku ya Jumapili.

"👀👀👀👁️😂" Jorginho aliandika kwenye picha ambayo alichapisha kwenye mtandao wa  Instagram.

Katika picha hiyo, Jorginho na Kai Havertz walionekana wenye furaha na tabasamu kubwa kwenye nyuso zao.

Arsenal inaripotiwa kuwa tayari imekamilisha usajili wa winga Kai Havertz kutoka Chelsea kwa takriban pauni milioni 65. (Ksh 11.6B).

Hata hivyo,Wanabunduki na Chelsea bado hawajathibitisha uhamisho huo kwa mashabiki wao kwenye mitandao rasmi.

Havertz anahamia Emirates miezi michache tu baada ya Jorginho kukamilisha uhamisho wake kwa dau la pauni milioni 12. (Ksh 2.1 bilioni).

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 31 alikabidhiwa jezi nambari 20 na alihusika katika mechi kadhaa za klabu hiyo ya Kaskazini mwa London katika sehemu ya pili ya EPL msimu wa 2022/23 baada ya kujiunga nao mwezi Januari

Jorginho alitia saini mkataba wa miezi 18, na chaguo la kuongeza mwaka mmoja zaidi. Jorginho alikuwa ndani ya miezi sita ya mwisho ya mkataba wake na Chelsea, na aliachiliwa kuondoka baada ya The Blues kukamilisha uhamisho wa rekodi ya Uingereza kwa kiungo wa kati wa Benfica, Enzo Fernandez.