Jeki kwa Wanabunduki huku Saliba na Nelson wakiongeza mikataba yao

Saliba atavalia jezi nambari 2 kuanzia msimu ujao.

Muhtasari

•Wanabunduki walitangaza kwamba mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 22 amekubali kuongeza muda wake wa kusalia katika klabu hiyo hadi mwaka wa 2027.

•Reiss Nelson pia alifanya uamuzi wa kusalia katika klabu hiyo yenye maskani yake Kaskazini mwa London.

ameongeza mkataba wake na Arsenal hadi 2027
William Saliba ameongeza mkataba wake na Arsenal hadi 2027
Image: ARSENAL

Beki wa kati wa Arsenal William Saliba ameongeza mkataba wake na klabu hiyo yenye maskani yake jijini London.

Katika taarifa yake siku ya Ijumaa, Wanabunduki walitangaza kwamba mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 22 amekubali kuongeza muda wake wa kusalia katika klabu hiyo hadi mwaka wa 2027. Pia ana chaguo la kuongeza mkataba wake na mwaka mmoja mwingine.

Arsenal pia ilithibitisha mabadiliko ya nambari ya jezi ya beki huyo wa kati.

“Pamoja na kusaini mkataba mpya, William pia atavaa nambari ya jezi mpya kwa msimu ujao, akihamia nambari 2 kwa msimu wa 2023/24,”Arsenal ilitangaza kupitia tovuti yake rasmi.

Saliba alikuwa sehemu muhimu ya Arsenal katika msimu wa 2022/23, akicheza mechi 33 katika mashindano yote huku akifunga mara tatu na kusaidia mara moja kutoka nyuma.

Alisajiliwa na wanabunduk kutoka Klabu ya Ufaransa, St Etienne mwaka wa 2019 na amekuwa na safari yenye milima na mabonde kabla ya kushirikishwa kikamilifu kwenye kikosi cha kwanza msimu uliopita.

"Kusema kweli uamuzi ulikuwa rahisi," Saliba alisema baada ya kusaini mkataba wake, "kwa sababu nilikuwa na msimu mzuri sana msimu uliopita, lakini kwa bahati mbaya sikuumaliza kwa sababu ya majeraha. Kwa hivyo nataka zaidi. Nataka kucheza miaka zaidi kwa klabu hii ya ajabu. Bado sijafanikiwa chochote, kwa hivyo nataka kushinda kila kitu nikiwa na klabu hii.”

Saliba alikuwa akilengwa na vilabu vingine vikubwa kabla ya kuamua kusalia katika Emirates. Mkataba wake wa awali ulipaswa kumalizika mwaka ujao na Wanabunduki walilazimika kumshawishi kubaki au kumuuza ili wasimwache aende bure mwishoni mwa msimu ujao

Nyongeza ya mkataba wa Mfaransa huyo ilikuja siku moja baada ya winga Reiss Nelson pia kufanya uamuzi wa kusalia katika klabu hiyo yenye maskani yake Kaskazini mwa London.

Siku ya Alhamisi, Arsenal ilitangaza kwamba winga huyo wa Uingereza ametia saini mkataba mpya wa muda mrefu hivyo kuongeza muda wake wa kusalia katika klabu hiyo.