Mwanasoka wa zamani wa Man City Benjamin Mendy aondolewa hatia ya ubakaji

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 28 alishtakiwa kwa kumshambulia mwanamke mwenye umri wa miaka 24

Muhtasari

Mendy pia alishtakiwa kwa jaribio la kumbaka mwanamke mwingine, mwenye umri wa miaka 29, ambaye pia alisema kuwa alimdhalilisha nyumbani kwake miaka miwili kabla.

Mwanasoka wa zamani wa Man City Benjamin Mendy
Image: reuters

Mwanasoka wa zamani wa Manchester City Benjamin Mendy ameondolewa mashtaka ya kumbaka mwanamke na kujaribu kumbaka mwingine.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 28 alishtakiwa kwa kumshambulia mwanamke mwenye umri wa miaka 24 katika jumba lake la kifahari huko Mottram St Andrew, Cheshire mnamo Oktoba 2020.

Mendy pia alishtakiwa kwa jaribio la kumbaka mwanamke mwingine, mwenye umri wa miaka 29, ambaye pia alisema kuwa alimdhalilisha nyumbani kwake miaka miwili kabla.

Inakuja baada ya kuondolewa makosa sita ya ubakaji katika kesi ya awali mwezi Januari.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa aliangua kilio wakati hukumu ya kutokuwa na hatia ikisomwa na msimamizi wa mahakama kufuatia kesi iliyodumu kwa wiki tatu katika Mahakama ya Chester Crown.

Jopo la Mahakama la majaji 12 lilijadili kwa takriban saa tatu na dakika 15 kabla ya kufikia hitimisho hilo.

Jaji Steven Everett alisema: "Bw Mendy anaweza kuachiliwa kutoka kizimbani."

Mwanasoka huyo, ambaye mkataba wake na Manchester City ulimalizika mapema mwezi huu, aliondolewa katika kesi ya awali ya makosa sita ya ubakaji na shtaka moja la unyanyasaji wa kingono, unahuhusisha na wasichana wanne.

KWINGINEKO NI KUWA;

Nigeria yatangaza hali ya hatari ya uhaba wa chakula

 

Rais wa Nigeria Bola Tinubu ametangaza hali ya hatari kuhusu usalama wa chakula ili kukabiliana na mfumuko wa bei ya chakula unaoendelea.

Mikakati ya haraka, ya kati na muda mrefu imeundwa na serikali kukabiliana na uhaba huo.

Ikiwa ni pamoja na kutoa mbolea na nafaka kwa wakulima na kaya hadi kutoa jukumu la kutoa chakula na maji kwa Baraza la Usalama la Taifa.

Serikali inapanga kutenga fedha kutokana na kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta kusaidia sekta ya kilimo na kuanzisha Bodi ya Kitaifa ya Bidhaa ili kudhibiti na kuleta utulivu wa bei za vyakula.

Rais Tinubu alisisitiza malengo ya mipango ya kupunguza gharama za chakula, kukuza kilimo na kuzalisha fursa za ajira.

Katika chapisho kwenye ukurasa wake wa Twitter, Rais Tinubu alisema kwamba "mipango mipya itakabiliana na kupanda kwa gharama za chakula, kuimarisha kilimo, na kuongeza ajira".

"Hakuna atakayeachwa nyuma katika juhudi zetu za kuhakikisha chakula cha bei nafuu na kingi kwa kila Mnigeria," alitweet.

Mapema mwezi huo, gavana wa zamani wa kaskazini mwa Nigeria alielezea wasiwasi wake kwamba nchi hiyo inaweza kukabiliwa na shida ya chakula hivi karibuni kutokana na ujambazi Kaskazini.

Shirika la Fedha Duniani lilionya juu ya kuongezeka kwa bei ya vyakula na hatari kutokana na mafuriko na mbolea ghali.