Maguire atiririkwa na machozi akidhibitisha kupokonywa unahodha Man United

"Meneja leo ameniarifu anabadilisha nahodha. Alinieleza sababu zake na ingawa mimi binafsi nimekatishwa tamaa sana, nitaendelea kujitolea kila ninapovaa shati." - Maguire.

Muhtasari

• Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza alimshukuru aliyekuwa kocha wa United Ole Gunnar Solskjaer kwa kumuaminia na unahodha miaka mitatu na nusu iliyopita.

Harry Maguire adhibitisha kupokonywa unahodha wa United.
UNAHODHA Harry Maguire adhibitisha kupokonywa unahodha wa United.
Image: INSTAGRAM

Beki wa Manchester United Harry Maguire ambaye amekuwa nahodha wa timu hiyo kwa Zaidi ya miaka mitatu amedhibitisha kupokonywa kitambaa cha unahodha katika mabadiliko mapya ambayo yanafanywa na kocha mkuu Erik Ten Hag.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Maguire alisema kwamba japo alipokea taarifa hizo kwa kusikitika mno, lakini ndio hivyo maamuzi yameshafanywa ka kusema kwamba ataendelea kutia juhudi zake ili kuipigania nembo ya Manchester United.

“Baada ya mazungumzo na meneja leo ameniarifu anabadilisha nahodha. Alinieleza sababu zake na ingawa mimi binafsi nimekatishwa tamaa sana, nitaendelea kujitolea kila ninapovaa shati. Kwa hivyo nilitaka kusema asante sana kwa mashabiki wa Manchester United kwa sapoti yao nzuri wakati nimekuwa nikivaa kitambaa,” Maguire aliandika.

Maguire alipokezwa unahodha miaka mitatu na nusu iliyopita na aliyekuwa kocha wa United, Ole Gunnar Solskjaer na amekuwa akipokea kashfa nyingi na masimango kutoka kwa mashabiki haswa kutokana na makosa yake mengi ambayo anafanya uwanjani – makosa ambayo husababisha United kufungwa na wengi wanahisi kwamba ni makosa yanayoweza kuepukika.

“Tangu siku nilipochukua jukumu hilo, miaka mitatu na nusu iliyopita, imekuwa ni fursa nzuri sana kuiongoza Manchester United na mojawapo ya nyakati za kujivunia maishani mwangu hadi sasa. Ni moja ya heshima kubwa katika soka la klabu. Nimefanya kila niwezalo kusaidia United kuwa na mafanikio - ndani na nje ya uwanja,” aliongeza.

Maguire alimshukuru Solskjaer kwa kumuaminia na unadhodha wa timu hiyo yenye historia ndefu, na kudokeza kwamba licha ya kuwepo kwa tetesi za kupoteza matumaini katika kikosi cha kwanza cha United, bado atazidi kujitolea kwa hali na mali kuitumikia timu hiyo.

“Nitamshukuru Ole Gunnar Solskjaer kwanza kwa kunipa jukumu hilo na ninamtakia yeyote atakayechukua hatua hiyo kwa kila mafanikio na watakuwa na usaidizi wangu kamili,” Maguire aliandika.