Riyad Mahrez aondoka City, kujiunga na Saudia

Ameenda zake kusaka muda zaidi wa kucheza na kula unono

Muhtasari

•Alichezea Manchester City mara 236 na kushinda mataji manne katika ligi ya Premier na moja ya UEFA.

Image: Riyad Mhrez// TWITTER

Aliyekuwa winga wa Manchester City Riyad Mahrez ametangaza rasmi kujiunga na klabu ya Al Ahli ya bara Asia katika uhamisho wa kudumu.

Mahrez amejiunga na ligi hiyo kutoka Manchester City, kwa kima cha pauni milioni 30, kile ambacho alisema kuwa ni kusaka muda zaidi wa kucheza, kwani gwiji huyo alitofautiana kidogo na meneja wa City katika nafasi anayoichezea.

Mwanasoka huyo mwenye uraia wa Algeria alijiunga na vigogo hao wa Uingereza Julai 2018 kutoka Leicester City, ambapo ameshiriki mara 236 na kuifungia City mabao 78 katika mashindano ya ligi kuu Uingereza.

Mahrez alikuwa na mchezo wa juu katika fainali ya kwanza kwenye ligi ya mabingwa, ambapo alisaidia City kufuzu hadi fainali ingawa walipoteza shindano hilo dhidi ya Chelsea mwaka wa 2021.

Gwiji huyo pia msimu uliotangulia alikuwa na kibarua kuingoza City kuyanyakua mataji yote matatu, akiwa alifunga mabao yote matatu katika nusu fainali ya kombe la FA, kuisaidia klabu hiyo kufika hatua ya fainali.

Aidha, mshambulizi huyo alionekana kutofurahishwa na uamuzi wa mkufunzi Pep Guardiola, kwani alilalamika kutemwa nje katika fainali ya ligi ya mabingwa na vilevile katika fainali ya kombe la FA.

Chini ya ukufunzi wa Guardiola, Mahrez alichezeshwa kama kiungo katika mfumo mpya meneja huyo alivumbua msimu uliopita, ambapo walishirikiana na naodha aliyeondoka kwenda Barcelona Ilkay Gundogan kuimarisha safu ya kati na pia kufanya mashambulizi.