Marcelo aondoka uwanjani kwa kwi kwi baada ya kumvunja mwenzake

"Leo, nililazimika kupata wakati mgumu sana uwanjani. Nimemjeruhi mwenzangu bila kukusudia." Marcelo alichapisha kwenye kurasa zake mitandaoni baada ya mechi hiyo.

Muhtasari

• Si kwamba alikuwa Analia kwa kurambishwa nyekundu bali kutokana na athari ambayo aliiacha kwenye mguu wa Sanchez.

Marcelo akimjeruhi Sanchez.
Marcelo akimjeruhi Sanchez.
Image: Screengrab

Beki wa zamani wa Real Madrid ambaye sasa anachezea Fluminense ya nyumbani kwao Brazil Marcelo alilazimika kuondoka uwanjani kwa kilio baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumkanyaga na kumvunja vibaya mchezaji wa timu pinzani.

Katika picha na video za tukio hilo, Beki wa Argentinos Juniors, Luciano Sanchez alikanyagwa vibaya kwenye muundi wa mguu wake na beki Marcelo, jeraha lililomzolea Marcelo kadi nyekundu ua moja kwa moja.

Sanchez ambaye mguu wake ulionekana kuvunjika kabisa alipandishwa kwenye machera na kuondolewa nje, lakini Marcelo hakuweza kustahimili taswira hiyo.

Si kwamba alikuwa Analia kwa kurambishwa nyekundu bali kutokana na athari ambayo aliiacha kwenye mguu wa Sanchez.

Sanchez, 29, alipata jeraha hilo baya baada ya Marcelo kukanyaga mguu wake bila kukusudia wakati akijaribu kusonga mbele na mpira, ESPN waliripoti.

Tukio hilo lilitokea katika dakika ya 56 ya mchezo huo ambao ulimalizika kwa sare ya 1-1.

Baada ya mchezo huo Marcelo alichapisha kwenye mtandao wa kijamii: "Leo, nililazimika kupata wakati mgumu sana uwanjani. Nimemjeruhi mwenzangu bila kukusudia. Nataka kukutakia ahueni bora zaidi Luciano Sanchez. Nakutumia nguvu zote duniani upate nafuu!"