Harry Kane ajawa bashasha baada ya kuhamia Bayern, asema ana hamu kubwa ya kushinda

Kane alisema kuwa ana furaha kubwa kuhamia klabu hiyo aliyoitaja kuwa moja ya klabu kubwa duniani.

Muhtasari

•Kane amejiunga rasmi na Bayern Munich kutoka Tottenham Hotspurs katika dili ambayo inaweza kupanda hadi pauni milioni 100 nyongeza zikijumuishwa.

•Mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy alifichua walijaribu sana kumpa Kane mkataba mpya lakini akasisitiza kwamba anataka changamoto mpya.

 

Image: TWITTER// BAYERN MUNICH

MSHAMBULIAJI Harry Kane amejiunga rasmi na Bayern Munich kutoka Tottenham Hotspurs katika dili ambayo inaweza kupanda hadi pauni milioni 100 nyongeza zikijumuishwa.

Bayern ilitangaza usajili wa mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza mwenye umri wa miaka 30 siku ya Jumamosi asubuhi na kufichua kwamba amesaini mkataba wa miaka 4 hadi 2027.

Kane atavaa jezi namba 9 katika klabu yake mpya na kuna matarajio mengi kutoka kwake kuhusu ufungaji mabao.

"Mshambulizi huyo wa Uingereza mwenye umri wa miaka 30 amekubaliana mkataba na mabingwa wa Ujerumani hadi tarehe 30 Juni 2027 na atavaa jezi namba 9 katika klabu ya Munich," Bayern ilisema kupitia tovuti yake rasmi.

Rais wa Bayern, Herbert Hainer alimkaribisha mfungaji huyo bora wa muda wote wa Tottenham katika mabingwa hao wa Bundesliga 2022/23 na kueleza imani yake kwamba mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza ataimarisha kikosi chake.

Kwa upande wake, Kane alisema kuwa ana furaha kubwa kuhamia klabu hiyo aliyoitaja kuwa moja ya klabu kubwa duniani.

"Nina furaha sana kuwa sehemu ya FC Bayern sasa. Bayern ni moja ya klabu kubwa duniani, na nimekuwa nikisema kila mara kuwa nataka kushindana na kujidhihirisha katika kiwango cha juu wakati wa uchezaji wangu. Klabu hii inajulikana na mawazo yake ya kushinda - najisikia vizuri sana kuwa hapa," Harry Kane alisema.

Mshambulizi huyo mwenye umri wa miaka 30 alifurahia mapokezi mazuri aliyopokea Bayern na alibainisha kuwa ana hamu sana ya kuanza kuichezea.

Huku wakimuaga mfungaji bora wao wa muda wote, Tottenham walimsherehekea kama gwiji na kumtakia heri katika maskani yake mapya.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Daniel Levy alifichua kwamba walijaribu sana kumpa Kane mkataba mpya lakini akasisitiza kwamba anataka changamoto mpya.

"Ningependa kumshukuru Harry kwa kila kitu alichotufanyia, kumbukumbu zote, rekodi zote - tunamtakia yeye na familia yake kila la heri kwa siku zijazo. Ni wazi kwamba anakaribishwa kila wakati tena. Anapendwa sana na Mwanachama wa thamani wa familia ya Spurs, milele katika historia yetu,” Levy alisema.

Harry Kane alijiunga na akademi ya Tottenham Football mnamo 2009 kabla ya kucheza mechi yake ya kwanza ya kulipwa mwaka 2015. Alicheza mechi 435 akiwa na Spurs na kufunga jumla ya mabao 280.