Christiano Ronaldo ashindwa kuficha furaha baada ya kushinda taji la kwanza na Al Nassr

Mshambuliaji huyo wa Ureno alifunga mabao mawili ya ushindi kabla ya kutolewa uwanjani baada ya kupata jeraha katika dakika za nyongeza.

Muhtasari

•Al Nassr ilishinda Kombe la King Salman Clubs Cup ikiwa na wachezaji 10 uwanjani, kwa hisani ya mabao mawili ya nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ureno.

•Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ureno hata hivyo hakuweza kumaliza mechi hiyo kwani alipata jeraha katika dakika ya 115.

Image: TWITTER// CHRISTIANO RONALDO

Christiano Ronaldo alishinda kombe lake la kwanza akiwa na klabu yake ya sasa ya Al Nassr Jumamosi jioni kufuatia ushindi wa 2-1 dhidi ya Al Hilal kwenye Uwanja wa King Fahd.

Al Nassr ilishinda Kombe la King Salman Clubs Cup ikiwa na wachezaji 10 uwanjani, kwa hisani ya mabao mawili ya nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ureno.

Kipindi cha kwanza cha mechi hiyo kiliisha bila bao kabla ya Al Hilal kutangulia kufunga katika dakika ya 51 baada ya kiungo Mbrazil Michael kumalizia pasi ya Malcom.

Masaibu zaidi yalifuata upande wa Ronaldo huku beki Abdulelah Al Amri akionyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 70. Dakika tatu baadaye hata hivyo, nyota huyo wa zamani wa Manchester United na Real Madrid alifufua matumaini ya Al Nassr kwa kufunga bao zuri.

Dakika 90 za kawaida za mechi hiyo zilimalizika kwa sare ya 1-1 na hivyo kumaanisha kwamba ilitakiwa kwenda hadi dakika za nyongeza. Haikuchukua muda mrefu kabla ya Christiano kufunga bao la pili la Al Nassr katika dakika ya 98.

Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ureno hata hivyo hakuweza kumaliza mechi hiyo kwani alipata jeraha katika dakika ya 115.

Mechi hiyo ilimalizika kwa mabao 2-1 na ushindi huo kuelekea upande wa Christiano ambao sasa umejawa na mastaa wengi wa soka.

Katika taarifa yake baada ya mechi hiyo, Christiano alieleza fahari yake baada ya kuisaidia Al Nassr kutwaa taji la King Salman Clubs Cup kwa mara ya kwanza.

"Asante kwa kila mtu katika kilabu ambaye alihusika katika mafanikio haya makubwa na kwa familia yangu na marafiki kwa kuwa karibu nami kila wakati! Sapoti ya ajabu kutoka kwa mashabiki wetu!Hii pia ni yako!," Christiano alisema.

Mashindano ya King Salman Clubs Cup yanachezwa na vilabu vya juu vya Kiarabu katika eneo hilo na yalijumuisha timu kutoka Saudi Arabia, Qatar, UAE, Iraq, Morocco, Tunisia na Algeria.