Fahamu faida Rwanda itavuna kutoka kwa mkataba wa 'Visit Rwanda' na Bayern Munich

Bayern Munich inakuwa klabu ya tatu ya Ulaya kusaini ushirikiano na Rwanda baada ya taifa hilo la Afrika Mashariki kusaini ushirikiano na Arsenal mwaka 2018, kisha na PSG mwaka uliofuata.

Muhtasari

• Klabu itaonyesha chapa ya Visit Rwanda kwenye skrini za LED za siku ya mechi katika ukumbi wa Allianz Arena wenye uwezo wa kuchukua watu 75,000.

Rwanda yaingia mkataba na Bayern Munich
Rwanda yaingia mkataba na Bayern Munich
Image: X

Taifa la Rwanda linaendelea kutangaza utamaduni na utalii wake ughaibuni kwa kutumia vilabu vya soka ambapo sasa wamefanikisha kuingia kwenye miadi na klabu ya tatu ya soka kaitka kuipeperusha falsafa ya utalii wao ya ‘Visit Rwanda’.

Baada ya falsafa hiyo kuwazolea faida nyingi kutokana na timu ya Arsenal na PSG, Rwanda sasa wamesaini mkataba na klabu ya Bayern Munich ambapo klabu hiyo itakwua inavaa jezi zenye nembo ya ‘Visit Rwanda’ mgongoni chini ya namba za jezi.

Kulingana na taarifa hiyo iliyochapishwa kwenye tovuti ya Bayern Munich, ushirikiano wao wa kibiashara utakwenda kwa miaka mitano hadi mwaka 2028.

Ushirikiano huo, uliozinduliwa wakati wa mechi ya kwanza ya FC Bayern ya nyumbani msimu huu, utashuhudia klabu hiyo ikifanya kazi mahususi na Wizara ya Michezo ya Rwanda kuanzisha chuo cha soka ili kuimarisha maendeleo ya soka nchini.

Zaidi ya hayo, klabu itaonyesha chapa ya Visit Rwanda kwenye skrini za LED za siku ya mechi katika ukumbi wa Allianz Arena wenye uwezo wa kuchukua watu 75,000 na shughuli mbalimbali zitaandaliwa ili kukuza utalii na fursa za uwekezaji nchini Rwanda, taarifa ilisoma kwenye tovuti.

Jan-Christian Dreesen, Afisa Mkuu Mtendaji wa FC Bayern, alisema: "Nimefurahishwa sana na ushirikiano huu uliokubaliwa hadi msimu wa joto wa 2028. FC Bayern inaweza kuwa hai katika bara la Afrika na kukusanya uzoefu muhimu. Ubia mpya wa platinamu unaendana na malengo ya muda mrefu. Tutakuza 'Visit Rwanda' na kuisaidia Rwanda kukua katika michezo na miradi ya soka la vijana. Hizi ni kazi zenye changamoto na uwajibikaji. Afrika ni bara la fursa. Kwa FC Bayern,hii ni hatua nyingine muhimu katika uwekaji wa kimataifa."

Aurore Mimosa Munyangaju, Waziri wa Michezo wa Rwanda alisema: "Tunafuraha kushirikiana na FC Bayern kusaidia maendeleo ya soka la vijana kwa wavulana na wasichana nchini Rwanda. Tunatazamia kuanzisha Chuo cha FC Bayern ambapo makocha wao wataalam kubadilishana ujuzi wa mchezo huo na makocha na wachezaji wazawa. Uwezo upo kwa Wanyarwanda kufanya vyema katika soka na ushirikiano huu unatoa jukwaa kubwa kwa Rwanda kujitahidi kupata ubora katika michezo."

Bayern Munich inakuwa klabu ya tatu ya Ulaya kusaini ushirikiano na Rwanda baada ya taifa hilo la Afrika Mashariki kusaini ushirikiano na Arsenal mwaka 2018, kisha na PSG mwaka uliofuata.