Anthony wa Man U aondolewa kwenye kikosi cha Brazil kufuatia madai ya kumshambulia ex wake

Cavallin alimshtumu kwa kumshambulia mara kadhaa na kumsababisha madhara ya mwili ikiwa ni pamoja na kwenye matiti na kidole.

Muhtasari

•Katika taarifa, timu ya taifa ya Brazil ilisema kuwa nia ya kumuondoa mchezaji huyo wa zamani wa Ajax kwenye kikosi ni kumlinda mwathiriwa.

•Cavallin alidai kuwa Antony alishambuliwa kwa mara ya kwanza nchini Brazil mnamo Juni 1 2022 akiwa mjamzito walipokuwa likizoni

Anthony
Image: HISANI

Winga wa Manchester United Anthony Matheus dos Santos hataiwakilisha nchi yake ya Brazil katika mechi zijazo hivi karibuni za kimataifa.

Hii ni kuhusiana na madai ya unyanyasaji wa nyumbani ambayo mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 23 ameshtumiwa na mpenzi wake wa zamani Gabriela Cavallin.

Katika taarifa, timu ya taifa ya Brazil ilisema kuwa nia ya kumuondoa mchezaji huyo wa zamani wa Ajax kwenye kikosi ni kumlinda mwathiriwa.

“Kutokana na ukweli uliojidhihirisha hadharani Jumatatu hii (Septemba 4), ukimhusisha mshambuliaji Antony, kutoka Manchester United, na ambao unatakiwa kuchunguzwa, na ili kumhifadhi mwathiriwa, mchezaji, timu ya Brazil na CBF, shirika linaarifu kwamba mwanariadha huyo ameondolewa katika timu ya Brazil,” taarifa ya timu ya taifa ya Brazil ilisoma.

Kujaza nafasi yake, Kocha Fernando Diniz alimuita Gabriel Jesus wa Arsenal, ambaye alichaguliwa kabla ya orodha ya wachezaji 36 iliyotumwa kwa  FIFA.

Katika shutuma zake, Bi Gabriela Cavallin anadai kwamba Antony alimshambulia mara kadhaa kati ya Juni 2022 na Mei mwaka huu.

Katika mahojiano na UOL, DJ huyo alidai kuwa Antony alishambuliwa kwa mara ya kwanza nchini Brazil mnamo Juni 1 2022 akiwa mjamzito walipokuwa likizoni . Anadai alitishia kumtupa kutoka kwa gari linaloenda.

Cavallin pia anadai Anthony alimpiga kwa kichwa na ngumi katika chumba cha hoteli ya Manchester mnamo Januari 15 2023 ambayo ilimsababishia madhara kwenye matiti. Anadai pia alipata jeraha la kidole wakati wa shambulio la Mei 8, 2023.

Anthony hata hivyo amekanusha madai hayo ambayo ameyataja kuwa ya uongo.

Katika taarifa yake kwenye Instagram, mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 23 alisema kuwa tuhuma hizo ziko chini ya uchunguzi na akaeleza imani yake kuwa hana hatia.

“Kwa heshima kwa mashabiki wangu, marafiki na familia ninahisi kuwajibika kuzungumza hadharani kuhusu mashtaka ya uwongo ambayo nimekuwa mwathiriwa. Tangu mwanzo nimelishughulikia suala hili kwa umakini na heshima, nikitoa ufafanuzi unaostahili kwa mamlaka ya polisi. Uchunguzi wa polisi uko chini ya ulinzi wa haki, na kwa hivyo siwezi kuweka maudhui yake hadharani,” Anthony alisema.

Aliongeza, “Hata hivyo, naweza kusema kwa kujiamini kwamba tuhuma hizo ni za uongo na kwamba ushahidi uliotolewa na unaotolewa zaidi unaonyesha kwamba sina hatia katika tuhuma zinazotolewa. Uhusiano wangu na Bi. Gabriela ulikuwa wa misukosuko, na vita vya maneno kutoka pande zote mbili, lakini sikuwahi kufanya uvamizi wowote wa kimwili. Kila wakati, iwe katika ushuhuda au katika mahojiano, anawasilisha toleo tofauti la mashtaka.”