Anthony wa Man United arejea mazoezini, akubaliwa kucheza huku uchunguzi wa polisi ukiendelea

Man U imesema ataendelea kushirikiana na polisi huku kesi iliyowasilishwa na ex wake Gabriela Cavallin ikiendelea.

Muhtasari

•Man U ilibainisha kuwa Anthony amekuwa akishirikiana vyema na polisi tangu Juni wakati madai ya dhuluma na unyanyasaji yalitolewa.

• Alhamisi, winga huyo mwenye umri wa miaka ishirini alijiwasilisha kwenye kituo cha polisi ambapo alihojiwa kwa saa kadhaa.

Image: HISANI

Klabu ya soka ya Uingereza, Manchester United imetangaza kurejea mazoezini kwa Anthony, takriban wiki mbili na nusu baada ya kumtenga winga huyo mwenye umri wa miaka 23.

Katika taarifa yake Ijumaa alasiri, klabu hiyo ya EPL ilibainisha kuwa Anthony amekuwa akishirikiana vyema na polisi tangu mwezi Juni wakati ambapo madai ya dhuluma na unyanyasaji yalipotolewa dhidi yake kwa mara ya kwanza.

Klabu hiyo pia ilibainisha kuwa mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil bado ataendelea kushirikiana na polisi nchini Uingereza na katika nchi yake ya nyumbani huku kesi iliyowasilishwa na aliyekuwa mpenzi wake Gabriela Cavallin ikiendelea.

"Kama mwajiri wa Antony, Manchester United imeamua kwamba ataanza tena mazoezi huko Carrington, na atapatikana kwa kuchaguliwa kwenye kikosi, wakati uchunguzi wa polisi ukiendelea. Hili litaendelea kuangaliwa ikisubiriwa maendeleo zaidi katika kesi hiyo,” ilisema taarifa ya klabu ya Manchester United.

Ilisema zaidi, "Kama klabu, tunalaani vitendo vya dhuluma na unyanyasaji. Tunatambua umuhimu wa kuwalinda wale wote wanaohusika katika hali hii, na tunakubali athari za madai haya kwa waathirika wa unyanyasaji."

Siku ya Alhamisi, winga huyo mwenye umri wa miaka ishirini na tatu ambaye ameshtakiwa kwa madai ya dhuluma na unyanyasaji na aliyekuwa mpenzi wake, Gabriella Cavallin alijiwasilisha kwenye kituo cha polisi nchini Uingereza ambapo alijibu maswali kuhusiana na kesi dhidi yake kwa saa kadhaa.

Mapema mwezi huu, United ilitangaza kwamba Anthony hangerejea kwenye mazoezi pamoja na wachezaji wengine ambao hawakushiriki mechi za kimataifa na badala yake angechelewesha kurejea kwa muda.

Klabu ilidokeza kuwa winga huyo alitarajiwa kujieleza kuhusu tuhuma zinazomkabili kabla ya kuruhusiwa kurejea klabuni.

“Manchester United inatambua madai yaliyotolewa dhidi ya Antony. Wachezaji ambao hawajashiriki katika mechi za kimataifa wanatarajiwa kurejea mazoezini Jumatatu. Hata hivyo, imekubaliwa na Antony kwamba atachelewesha kurejea kwake hadi taarifa nyingine ili kushughulikia madai hayo,” Man United ilisema.