•PGMOL ilikiri kwamba kukataa bao la Luis Diaz kwa madai ya kuotea katika dakika ya 34 ya mechi hiyo lilikuwa kosa la wazi.
•Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp alibainisha kuwa hatua hiyo haisaidii kwani hawatapata pointi yoyote baada yake.
Muungano wa Wasimamizi wa Mechi nchini Uingereza (PGMOL) umetoa taarifa wakikiri kwamba makosa makubwa yalitokea wakati wa kipindi cha kwanza cha mechi ya Tottenham dhidi ya Liverpool kwenye Uwanja wa Tottenham Jumamosi jioni.
Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi jioni, PGMOL ilikiri kwamba kukataa bao la Luis Diaz kwa madai ya kuotea katika dakika ya 34 ya mechi hiyo lilikuwa kosa la wazi.
Chama hicho cha marefa kilikubali kwamba bao la mshambuliaji huyo wa Colombia lilipaswa kukubaliwa baada ya ukaguzi wa VAR kwa uwezekano wa kuotea, jambo ambalo halikufanyika.
“Bao la Luis Diaz lilikataliwa kwa kuotea na mmoja wa wasimamizi wa mechi waliopo uwanjani. Hili lilikuwa kosa la wazi na la kweli na lilipaswa kufanya bao hilo kupewa kupitia uingiliaji wa VAR. Hata hivyo, VAR ilishindwa kuingilia kati,” ilisema taarifa ya PGMOL.
Muungano wa waamuzi uliahidi kufanya uhakiki kamili juu ya mazingira ambayo yalisababisha makosa hayo na kuchukua hatua muhimu baadaye.
Pia walitangaza kuwa watawasiliana na klabu ya Liverpool ili kukiri kosa hilo.
"PGMOL itawasiliana mara moja na Liverpool mwishoni mwa mechi ili kukiri makosa," ilisema taarifa hiyo.
Wakati akizungumzia taarifa ya PGMOL baada ya mechi kukamilika, kocha wa Liverpool Jurgen Klopp alibainisha kuwa hatua hiyo haisaidii vyovyote kwani hawatapata pointi yoyote baada yake.
"Tulikuwa na hali kama hiyo kwenye mchezo wa Man United, je Liverpool walipata pointi kwa hilo? Hapana. Naamini hatutapata pointi kwa hilo pia. Haisaidii,” Klopp alisema.
Aliongeza, "Hakuna anayetarajia maamuzi sahihi 100% uwanjani. Lakini nadhani sote tulifikiri kwamba VAR inapoingia, inaweza kurahisisha mambo. Sijui kwa nini watu na VAR waliweka mechi hiyo kwa presha. Uamuzi ulifanywa haraka sana naweza kusema kuhusu hilo. Natumaini aliyefanya hivyo, aliyefanya uamuzi, hakufanya makusudi. Hiyo ni ajabu lakini lazima mtu mwingine atoe ufafanuzi. Sina la kusema,."
Liverpool walipoteza kwa Tottenham 2-1 Jumamosi jioni baada ya wachezaji wao wawili kutolewa nje kwa kadi nyekundu wakati wa mechi. Bao la ushindi la Tottenham lilipatikana katika dakika za nyongeza baada ya mlinzi Joel Matip kujifunga.