Tottenham, Premier League wavunja kimya kuhusu ubaguzi wa rangi dhidi ya beki Destiny Udogie

Spurs wametangaza kuwa wanashirikiana na Ligi Kuu ili hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika.

Muhtasari

•Tottenham na EPL zimekashifu jumbe za ubaguzi wa rangi zilizoelekezwa kwa beki wa kushoto Destiny Udogie.

•Ligi Kuu ilieleza kuwa ubaguzi wa rangi au aina yoyote ya ubaguzi dhidi ya wachezaji hautavumiliwa hata kidogo.

Image: HISANI

Klabu ya soka ya Tottenham Hotspurs na Ligi Kuu ya Uingereza zimekashifu jumbe za ubaguzi wa rangi zilizoelekezwa kwa beki wa kushoto Destiny Udogie.

Mwanasoka huyo wa maika 20 mwenye kipawa kikubwa amekuwa akipokea jumbe baya kwenye mitandao ya kijamii kufuatia ushindi wa Tottenham wa mabao 2-1 dhidi ya Liverpool siku ya Jumamosi. Alikuwa mmoja wa wachezaji bora uwanjani wakati wa mechi hiyo iliyochezwa kwenye uwanja wa Tottenham Hotspurs lakini inaonekana si kila mtu alifurahishwa na uchezaji wake kulingana na jumbe hasi alizopokea kwenye mitandao ya kijamii.

Tottenham imesema klabu  imechukizwa na jumbe hizo za kibaguzi na wametangaza kuwa wanashirikiana na Ligi Kuu ili hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika.

"Tumechukizwa na jumbe za kibaguzi zinazoelekezwa kwa Destiny Udogie kwenye mitandao ya kijamii kufuatia mchezo wa Jumamosi dhidi ya Liverpool. Tutafanya kazi na Ligi Kuu na, inapowezekana, kuchukua hatua dhidi ya mtu yeyote ambaye tunaweza kumtambua. Tunasimama nawe Destiny,” Tottenham ilisema kwenye taarifa.

Ligi Kuu ya Uingereza kwa upande wao ilieleza kuwa ubaguzi wa rangi au aina yoyote ya ubaguzi dhidi ya wachezaji hautavumiliwa hata kidogo.

"Tutaendelea kufanya kazi pamoja na vilabu ili kuhakikisha kesi zinaripotiwa na kuchunguzwa na wahalifu wanakabiliwa na athari mbaya," taarifa ya Ligi Kuu ilisoma.

Ligi Kuu pia iliwashinikiza watu kupiga ripoti mara moja pindi matukio ya ubaguzi wa rangi yanapotokea.

Udogie ndiye mchezaji wa soka wa hivi majuzi kukabiliana na ubaguzi wa rangi wakati akitoa huduma zake kama mwanasoka wa kulipwa barani Ulaya. Wachezaji wengine wengi wameathirika huko nyuma huku hatua kali zikichukuliwa dhidi ya wakosaji huku baadhi ya kesi zikiisha bila kushughulikiwa.