"Ni wakati wa kufurahia na wapendwa!" Eden Hazard astaafu soka akiwa na miaka 32

Hazard alikua mchezaji huru tangu Juni 2023 wakati yeye na Real Madrid waliafikiana kusitisha mkataba wake.

Muhtasari

•Hazard alibainisha kuwa amejisikiliza na kugundua kuwa ni wakati mwafaka wa yeye kuondoka kwenye taaluma ya soka.

•Hazard alitoa shukrani za dhati kwa vilabu vyake vya zamani Lille, Chelsea na Real Madrid na bila kusahau timu ya soka ya Ubelgiji.

Image: INSTAGRAM// EDEN HAZARD

Kiungo wa kati wa  zamani wa Chelsea na Real Madrid,  Eden Hazard ametangaza kustaafu kucheza soka la kulipwa.

Katika taarifa yake Jumanne asubuhi, mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 32 alibainisha kuwa amejisikiliza na kugundua kuwa ni wakati mwafaka wa yeye kuondoka kwenye taaluma ya soka.

Mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Ubelgiji aliweka wazi kuwa anajivunia taaluma yake ya soka ya miaka 16 ambayo imemfanya acheze katika vilabu vitatu vikubwa katika nchi tatu tofauti za Ulaya.

"Lazima ujisikilize na kusema acha kwa wakati unaofaa. Baada ya miaka 16 na kucheza zaidi ya mechi 700, nimeamua kukatisha taaluma yangu kama mwanasoka wa kulipwa,” Hazard alisema katika taarifa yake Jumanne asubuhi.

Aliongeza, “Niliweza kutimiza ndoto yangu, nimecheza na kufurahiya kwenye viwanja vingi duniani. Wakati wa taaluma yangu, nilibahatika kukutana na wasimamizi wakubwa, makocha na wachezaji wenzangu - asante kwa kila mtu kwa nyakati hizi nzuri, nitawamiss nyote."

Hazard aliendelea kutoa shukrani za dhati kwa vilabu vyake vya zamani Lille, Chelsea na Real Madrid na bila kusahau timu ya soka ya Ubelgiji.

Pia hakukosa kuwashukuru familia yake, marafiki na mashabiki kwa kumuonyesha upendo katika maisha yake yote ya soka na kusimama naye kila wakati.

"Shukrani za kipekee kwa familia yangu, marafiki zangu, washauri wangu na watu ambao wamekuwa karibu nami katika nyakati nzuri na mbaya. Hatimaye, asante sana kwenu mashabiki wangu ambao mmekuwa mkinifuatilia kwa miaka yote hii na kwa kunitia moyo kila mahali nilipocheza. Sasa ni wakati wa kufurahia wapendwa wangu na kuwa na uzoefu mpya.Tuonane nje ya uwanja hivi karibuni marafiki zangu," alisema.

Hazard aliambatanisha taarifa hiyo na picha za matukio kadhaa ya kukumbukwa akiwa na vilabu vyake vitatu vya zamani na timu ya soka ya Ubelgiji.

Hazard alikua mchezaji huru tangu Juni 2023  wakati yeye na klabu yake ya zamani ya Real Madrid waliafikiana  kusitisha mkataba wake. Mbelgiji huyo bado alikuwa na mwaka mmoja kwenye mkataba wake na klabu hiyo ya Uhispania wakati alipoondoka.

Alishindwa kucheza vizuri nchini Uhispania na hakucheza mara nyingi kutokana na majeraha baada ya kuondoka Chelsea mnamo 2019.