Christiano Ronaldo kuchapwa mijeledi 99 kwa kum'hug mwanamke shabiki wake Iran

Kwa mujibu wa Mtandao wa Irani, Sharq Emroz, kumgusa au kukaribiana na mwanamke aliyeolewa ni sawa na uzinzi katika taifa hilo linalozingatia kwa umakini sheria za kidini za Kiislamu.

Muhtasari

• Inasemekana Ronaldo alimbusu shavuni na kumpa shati yenye saini, huku pia akipiga picha akiwa amemkumbatia jambo ambalo limewavutia wanasheria wa Iran.

• Alitembelea Tehran, mji mkuu wa Iran, akiwa na Al-Nassr kumenyana na Persepolis katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Asia mwezi Septemba.

Ronaldo akiwa na shabiki aliyemchora
Ronaldo akiwa na shabiki aliyemchora
Image: Screengrab

Cristiano Ronaldo huenda akakabiliwa na hukumu ya 'mijeledi 99 kwa uzinzi' wakati mwingine atakapozuru Iran kwa sababu ya picha yake na mchoraji, kulingana na ripoti nchini humo.

Vyombo vya habari vya Iran, kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo, vimedai kuwa idadi kubwa ya mawakili nchini humo wamewasilisha malalamiko juu ya nyota huyo wa Al-Nassr kutokana na picha ambayo ilipigwa katika ziara yake huko nyuma mwezi wa Septemba.

Ronaldo ambaye yuko kwenye uhusiano na mwanamitindo wa Uhispania Georgina Rodriguez, alitembelea Tehran, mji mkuu wa Iran, akiwa na Al-Nassr kumenyana na Persepolis katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Asia mwezi Septemba.

Akiwa huko, mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno alikutana na mchoraji wa Iran, Fatima Hamimi, ambaye alitaka kumpa picha nyota huyo wa zamani wa Manchester United na Real Madrid, ambayo alimtengenezea hasa.

Inasemekana Ronaldo alimbusu shavuni na kumpa shati yenye saini, huku pia akipiga picha akiwa amemkumbatia jambo ambalo limewavutia wanasheria wa Iran.

Hii ni kwa sababu katika sheria za Iran, kumgusa mwanamke aliyeolewa ni sawa na uzinzi.

Hamimi anasemekana kuwa 'asilimia 85 amepooza' na ni shabiki mkubwa wa nyota huyo wa Ureno.

Mtandao wa Irani, Sharq Emroz, kama ilivyo kwa Mundo Deportivo, unasema kwamba mfumo wa haki wa Iran uliitikia haraka picha ya wawili hao na kumhukumu Ronaldo kuchapwa viboko 99 wakati mwingine aliposafiri kwenda Iran.

Al-Nassr wanashiriki katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Asia ambapo wapo Kundi E pamoja na Persepolis ya Iran, Al-Duhail ya Qatar na Istiklol ya Takikistan.

Hatarejea Iran katika awamu hii ya mashindano lakini iwapo wangefanya hatua ya mtoano, haiwezi kuzuiliwa kuwa itamlazimu kukanyaga tena ardhi ya Iran.

Inasemekana kwamba akifanya hivyo, Ronaldo anaweza kukamatwa na mamlaka nchini Iran ili kumlazimisha kutumikia kifungo hicho.

Walakini, kama ilivyoripotiwa na Marca, hukumu hiyo inaweza kusamehewa na jaji ikiwa 'vitendo haviwezi kuadhibiwa au Ronaldo akionyesha majuto'.