Babake Luis Diaz alemewa na hisia huku akimtazama mwanawe akiifungia Colombia mabao mawili (+video)

Diaz aliifungia Colombia mabao mawili ndani ya dakika tatu tu kuelekea robo ya mwisho ya mechi kali dhidi ya Brazil.

Muhtasari

•Babake Diaz alishindwa kujizuia huku mwanawe akifunga mabao mawili dhidi ya timu ya taifa ya Brazil na kuipa Colombia  ushindi muhimu.

•Diaz alisema ushindi huo na mabao yake yanamwendea baba yake ambaye alipitia kipindi cha kutisha siku chache zilizopita.

alemewa na hisia baada ya mwanawe kufunga mabao mawili.
Luis Manuel Dias Sr alemewa na hisia baada ya mwanawe kufunga mabao mawili.
Image: HISANI

Baba ya mshambulizi Luis Diaz, Luis Manuel Dias Sr alishindwa kujizuia usiku wa kuamkia Ijumaa alipomtazama mwanawe akifunga mabao mawili dhidi ya timu ya taifa ya Brazil na kuipa Colombia  ushindi muhimu katika mashindano ya kufuzu Kombe la Dunia la 2026.

Diaz aliifungia nchi yake mabao mawili ndani ya dakika tatu tu kuelekea robo ya mwisho ya mechi kali dhidi ya Brazil ambao wameorodheshwa katika nafasi ya tatu duniani. Mechi hiyo ilichezwa kwenye Uwanja wa Estadio Metropolitano Roberto Melendez mjini Barranquilla, Colombia mwendo wa saa tisa usiku wa kuamkia Ijumaa.

Baba ya Diaz ambaye hivi majuzi alitumia takriban siku kumi na mbili mikononi mwa watekaji nyara alikuwemo uwanjani pampja na maelfu ya mashabiki wengine wakati winga huyo wa Liverpool akiipa nchi yake ushindi nyumbani.

Video ambazo zimesambaa kwenye mtandao ya kijamii zinamuonyesha Bw Manuel Diaz Sr akilia kwa hisia huku akishikiliwa na mashabiki wengine baada ya mwanawe kufunga mabao mawili dhidi ya mlinda lango wa Brazil Allison Becker. Uwanja mzima ulijaa kelele za kusherehekea huku Bw Manuel akitumia machozi ya furaha kueleza hisia zake.

Baada ya mechi hiyo, Luis Diaz alisema ushindi huo na mabao yake yanamwendea baba yake ambaye alipitia kipindicha kutisha siku chache zilizopita.

"Nilikuwa nikimfikiria baba yangu muda wote uwanjani, kila mara alikuwa na mawazo sahihi katika nyakati ngumu," Luis Diaz aliwaambia waandishi wa habari.

Aliongeza, "Ushindi huu, mabao haya yanaenda kwake."

Wanamgambo wa ELN walimkabidhi Luis Manuel Diaz kwa waumini wa kanisa katoliki na Umoja wa Mataifa Alhamisiwiki iliyopita, kumaliza takriban wiki mbili za wasiwasi wa kimataifa kuhusu hali yake na mahali alipo.

Manuel Diaz Sr alikuwa amezuiwa kwa siku 13 baada ya kutekwa nyara na kikundi cha waasi cha ELN, kwenye kituo cha mafuta cha Colombia karibu na mpaka na Venezuela mwishoni mwa mwezi uliopita.

Mama wa mchezaji huyo pia alikuwa ametekwa nyara katika tukio hilo lililotokea Oktoba 28 lakini aliokolewa ndani ya saa chache baada ya polisi kuweka vizuizi barabarani.

Ripoti za awali zilidai kuwa alitekwa nyara na mafia wa eneo hilo lakini utambulisho halisi wa waliomteka nyara ulifichuliwa tarehe Novemba 2 wakati timu ya maafisa wa serikali waliokuwa wakijadiliana na makundi ya waasi wenye silaha walisema ELN, kundi kongwe zaidi la waasi nchini humo ndilo lilikuwa limemshikilia mateka.