Benjamin Mendy aishtaki ManCity kwa kutomlipa takribani shilingi bilioni 2

"Manchester City FC ilishindwa kumlipa Bw Mendy ujira wowote kuanzia Septemba 2021, kufuatia Bw Mendy kushtakiwa kwa makosa mbalimbali ambayo yote aliachiliwa huru."

Muhtasari

• Manchester City hawakuzungumza lolote walipotafutwa na Sky Sports News

• Mendy alikua mlinzi ghali zaidi katika Premier League wakati City ilipolipa £52m kwa Monaco kwa ajili yake mwaka 2017.

Benjamin Mendy
Benjamin Mendy
Image: PA MEDIA

Benjamin Mendy amezindua madai ya "mamilioni kadhaa" dhidi ya Manchester City juu ya kutolipwa mishahara, runinga ya habari za kimichezo, Sky Sports News imebaini.

Beki huyo wa zamani wa City mwenye umri wa miaka 29 amewasilisha madai hayo kwenye Mahakama ya Ajira ndani ya siku chache zilizopita, akidai "makato yasiyoidhinishwa ya mshahara" baada ya kushtakiwa kwa ubakaji na unyanyasaji wa kingono mwaka wa 2021.

Mnamo Julai, Mendy alipatikana na mahakama bila hatia katika kesi iliyosikilizwa tena katika Mahakama ya Chester Crown.

Mapema mwaka huu mwanasoka huyo alikutwa hana hatia ya dhuluma za kingono dhidi ya wanawake kadhaa lakini jopo la mahakama halikuweza kufikia uamuzi wa mashtaka hayo mawili, na kusababisha kesi hiyo kusikizwa tena.

Mendy amekuwa akitaka kurejeshewa malipo anayodaiwa hadi mwisho wa mkataba wake uliomalizika Juni 2023.

Nick De Marco KC amethibitisha kwa Sky Sports News kuwa anakaimu kwa niaba ya mchezaji huyo wa sasa wa Lorient, na kwamba madai yamewasilishwa.

Taarifa ilisema: "Nick De Marco KC (aliyeagizwa na Laffer Abogados (Madrid) anakaimu nafasi ya mchezaji wa zamani wa Manchester City Benjamin Mendy katika madai ya mamilioni ya pauni kwa kukatwa mishahara bila kibali.

"Manchester City FC ilishindwa kumlipa Bw Mendy ujira wowote kuanzia Septemba 2021, kufuatia Bw Mendy kushtakiwa kwa makosa mbalimbali ambayo yote aliachiliwa huru, hadi mwisho wa mkataba wake Juni 2023. Madai hayo yatawasilishwa mbele ya mahakama Mahakama ya Ajira."

Manchester City hawakuzungumza lolote walipotafutwa na Sky Sports News

Mendy alikua mlinzi ghali zaidi katika Premier League wakati City ilipolipa £52m kwa Monaco kwa ajili yake mwaka 2017.

Alishinda mataji matatu akiwa na City na alikuwa sehemu ya kikosi cha Ufaransa kilichoshinda Kombe la Dunia mwaka 2018.

Mendy aliichezea klabu hiyo mara ya mwisho Agosti 2021, na sasa anachezea Lorient katika Ligue 1.