AFCON 2023: Wenyeji Ivory Coast wawabandua watetezi Senegal baada ya kupewa uhai mpya

Wenyeji sasa watamenyana na D.R Congo au Guinea kwenye robo fainali.

Muhtasari

•Ivory Coast waliwabandua nje mabingwa wa AFCON 2021 kupitia mikwaju ya penalti baada ya mechi kuisha kwa sare ya 1-1.

•Cape Verde pia iliikatisha tamaa Mauritania katika dakika za mwisho za pambano lao la saa mbili usiku wa Jumatatu.

waliwabandua Senegal kutoka Afcon
Ivory Coast waliwabandua Senegal kutoka Afcon
Image: HISANI

Wenyeji, Ivory Coast na Cape Verde waliungana na timu za Nigeria, D.R Congo, Guinea na Angola katika robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2023 (AFCON) baada ya kushinda mechi zao za hatua ya 16 bora siku ya Jumatatu usiku, Januari 29.

Ivory Coast ambao waliongozwa na kocha wa muda Emerse Fae usiku wa Jumatatu baada ya hivi majuzi kumtimua kocha mkuu Jean-Louis Gasset waliwabandua nje mabingwa wa AFCON 2021 kupitia mikwaju ya penalti baada ya mechi kuisha kwa sare ya 1-1.

Mshambulizi Habib Diallo alitangulia kuifungia Senegal katika dakika za mapema sana za mechi kabla ya kiungo wa kati wa Ivory Coast Franck Kessie kukatisha matumaini ya mabingwa hao watetezi kushinda tena kombe hilo kwa kusawazisha dakika ya 86.

Hii ilifanya mechi kwenda kwa muda wa ziada, kisha mikwaju ya penalti ambapo Ivory Coast ilifunga penalti zake zote tano huku Senegal ikikosa moja.

Wenyeji sasa watamenyana na D.R Congo au Guinea kwenye robo fainali.

Cape Verde pia iliikatisha tamaa Mauritania katika dakika za mwisho za pambano lao la saa mbili usiku wa Jumatatu.

Mauritania walikuwa wamecheza mchezo mzuri na kujilinda vyema lakini makosa ya kipa Babacar Niasse dakika ya 87 yaliipatia Cape Verde penalti iliyofungwa na fowadi Ryan Mendes. Bao hilo moja lilitosha kuipeleka Cape Verde katika hatua ya robo fainali ambapo itakutana na washindi wa mechi ya Morocco na Afrika Kusini itakayochezwa Jumanne usiku.

Tazama ratiba ya mechi za Jumanne;

Mali vs Burkina Faso (Saa mbili kamili usiku masaa ya Afrika Mashariki kwenye uwanja wa Amadou Gon Coulibaly, Korhogo)

Morocco vs Afrika Kusini (Saa tano kamili usiku masaa ya Afrika Mashariki kwenye uwanja wa Stade Laurent Pokou, San Pedro)