Wachezaji wasio weusi wana uwezekano wa hadi 50% kupata ukocha katika timu kuliko wachezaji weusi katika kipindi cha miaka 30, kulingana na utafiti wa Black Footballers Partnership (BFP).
Ripoti ya wasomi watatu iliangalia maisha ya nje ya uwanja ya takribani wanasoka 3,500 wa zamani waliocheza Ligi Kuu ya Uingereza au Klabu Bingwa kati ya 1990 na 2010.
Iligundua licha ya wachezaji weusi kuwa na 25% ya sifa za ukocha zilizotolewa na Uefa, 2022 na 2023, walichangia 4% pekee ya majukumu ya ukocha.
Delroy Corinaldi, mkurugenzi mtendaji wa BFP, anasema: "Kazi katika usimamizi wa soka mara nyingi inaonekana ni kazi inayoongeza watu, lakini kwa wachezaji wa zamani weusi, hawaongezeki katika kazi hiyo".
BFP ni shirika la wachezaji weusi waliopo na wa zamani.
Ripoti hiyo ilitoa muhtasari kwamba wachezaji wa zamani weusi hupata nafasi chache kwenye usimamizi, hupandishwa vyeo polepole zaidi, maendeleo yao hukwama haraka na hufukuzwa kazi haraka kuliko wenzao wasio weusi.
Pia ripoti hiyo ilieleza mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na:
Kocha mweusi ana uwezekano wa 41% kufutwa kazi kuliko kocha mzungu - wakati vipengele kama vile utendakazi ni sawa. Na katika majukumu yote ya usimamizi, mtu mweusi ana uwezekano wa 17% kufutwa kazi.
Kati ya wachezaji 3,500 katika utafiti huo, 73% ya wachezaji weusi walicheza Ligi Kuu ya Uingereza kwa wastani wa mechi 62 kwa kila mchezaji, huku 62% ya wachezaji wasio weusi walionekana kwenye ligi kuu, na wastani wa mechi 49.
"Matokeo ni ya kushangaza sana," Corinaldi aliambia shirika la habari la PA.
"Wachezaji kandanda wamekuwa kizazi kilichopotea nje ya uwanja, licha ya kuwa walikuwa nyota ndani ya uwanja."
Ripoti hiyo ilichapishwa muda mfupi baada ya kuthibitishwa kuwa serikali ya Uingereza itaanzisha msimamizi huru wa soka wakati Mswada wa Utawala wa Soka utakapowasilishwa Bungeni siku ya Jumanne.
Wachezaji wa zamani wakiwemo Les Ferdinand, Chris Ramsey, Michael Johnson, Ricky Hill, Paul Davis na Sol Campbell wamejiunga na wito wa Corinaldi – kutaka malengo ya ushirikishwaji na ujumuishwaji wa watu wa jamii mbalimbali yawemo katika Mswada wa Utawala wa Soka.
Pia wametoa wito kwa wadau wa soka kufanya kazi na BFP ili kuelewa ubaguzi katika mchezo huo na kwa wanasoka weusi kupata msaada wanaohitaji ili kujiendeleza kila ngazi ya mchezo bila kuzuiwa na chuki au ubaguzi wa rangi.
"Mdhibiti huru anaweza kutoa fursa lakini ikiwa hatashughulikia usawa wa rangi katika mchezo kulingana na data zinavyoonyesha basi itakuwa ni fursa iliyokwenda bure," aliongeza Corinaldi.
"Ripoti hii ni fursa kwa mchezo wa soka kujiunda upya, kushirikiana tena na BFP ili tufanye kazi kuelekea suluhisho endelevu."