Pigo kwa Man City huku mabeki watatu wakijeruhiwa kabla ya mechi kubwa dhidi ya Arsenal

John Stones, Manuel Akanji na Kyle Walker wote waliripotiwa kupata majeraha wakati wa mapumziko ya kimataifa.

Muhtasari

•John Stones alicheza kwa dakika tisa pekee katika mechi ya Jumanne usiku kabla ya kutolewa nje ya uwanja wa Wembley baada ya kuumia.

•Manuel Akanji aliripotiwa kujiondoa katika majukumu ya kimataifa ya Uswizi siku ya Jumatatu baada ya kupata jeraha lisilofichuliwa.

Image: INSTAGRAM// MAN CITY

Manchester City ilipata pigo lingine siku ya Jumanne jioni baada ya beki wa kati John Stones kuumia wakati wa mchuano wa Uingereza dhidi ya Ubelgiji.

Beki huyo mwenye umri wa miaka 29 alicheza kwa dakika tisa pekee katika mechi hiyo ya saa nne usiku kabla ya kutolewa nje ya uwanja wa Wembley baada ya kuumia. Nafasi yake ilichukuliwa na Joe Gomez wa Liverpool.

Jeraha la Stones lilileta wasiwasi zaidi kwa washindi wa EPL 2022/23 Man City kwani mabeki wengine wawili, Manuel Akanji na Kyle Walker pia walikuwa wameziaga timu zao za taifa kutokana na majeraha.

Manuel Akanji aliripotiwa kujiondoa katika majukumu ya kimataifa ya Uswizi siku ya Jumatatu baada ya kupata jeraha lisilofichuliwa.

Bosi wa Uswizi, Murat Yakin alifichua Jumatatu jioni kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 alikuwa amepata jeraha na hangeshiriki katika mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Ireland Jumanne.

Hapo awali, beki wa kulia Kyle Walker pia alikuwa ameondoka kwenye kambi ya Uingereza baada ya kuumia.

Shirika la Soka la Uingereza mnamo siku ya Jumapili lilithibitisha kwamba kipa Sam Johnstone, Harry Maguire na Kyle Walker waliondoka kambini na kurejea katika vilabu vyao kwa ajili ya kuchunguzwa baada ya kupata majeraha katika siku za hivi majuzi.

Timu ya taifa ya Uingereza iliwatakia ahueni ya haraka.

"Kyle Walker, Sam Johnstone na Harry Maguire wamerejea katika vilabu vyao kwa kutathmini kuwa wamepata majeraha katika siku za hivi karibuni. Tunawatakia ahueni ya haraka vijana," timu ya taifa ya Uingereza ilisema katika taarifa yake.

Tatizo la majeraha katika Man City linakuja siku chache tu kwa mechi yao kubwa dhidi ya Arsenal ambao wamekaa kileleni mwa jedwali.

Siku ya Jumapili, Arsenal itamenyana na timu ya Guardiola ikiwa na nafasi ya kwenda pointi nne mbele ya City katika mbio za kuwania taji la Ligi Kuu ya Uingereza.

Wanabunduki kwa sasa wanaongoza jedwali mbele ya Liverpool kwa tofauti ya mabao wakiwa na pointi 64, huku Man City wakishika nafasi ya tatu kwa pointi 63.