Raila Odinga apongeza Harambee Stars kwa kuwakaba koo Ivory Coast

Kenya iko katika nafasi ya 107 katika orodha ya FIFA ya dunia kwa wanaume huku miamba wa Afrika, Ivory Coast ikishikilia nafasi ya 38.

Muhtasari

•Waziri mkuu wa zamani,Raila Odinga amewapongeza wachezaji wa Harambee Stars baada ya kupiga sare tasa dhidi ya Ivory Coast kwenye mechi ya kufuzu kombe la dunia,2026

•Kenya inashikilia nafasi ya tatu kwa alama tano kwenye kundi F nyuma ya vigogo Ivory Coast na Gabon wanaoshikilia nafasi ya pili kwa alama sita.

Raila Odinga
Image: Hisani

 Aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga ameipongeza Harambee Stars baada ya kutoka sare tasa na Ivory Coast  katika mechi ya kufuzu kwa kombe la dunia 2026.

Matokeo hayo yanaonyesha  mafanikio makubwa kwa Stars, kwani ndiyo timu ya kwanza kusimamisha wababe hao, ambao wameeka ushindi  mara tatu mfululizo katika Kundi F.

Raila hakusita kuwamiminia sifa tele wachezaji wa Harambee Stars kutokana na kujituma kwao kwa mechi hio.Ujumbe wa pongezi wa Raila umewagusa wakenya wengi, na kuwatia moyo kujiamini na kujivunia kitaifa.

"Harambee Stars yetu ilionyesha shauku na ukakamavu wa ajabu nchini Malawi, na kupata sare ya 0-0 dhidi ya mabingwa wa Afrika, Ivory Coast. Tunajivunia ari na ukakamavu wa timu," Raila alisema.

Kwa sasa Kenya ipo katika nafasi ya tatu katika kundi F kwa alama tano, nyuma ya Gabon walio na sita, na Ivory Coast inayoongoza kwa alama 10. 

Safari ya kenya katika mchujo wa  kufuzu kwa kombe la dunia 2026 inaendelea kushika kasi.Azma na ari waliyoonyesha kwenye mchezo wao dhidi ya Ivory Coast imewapendeza mashabiki wengi.

Kocha Firat pia ,katika mahojiano baada ya mechi, aliangazia utofauti baina ya wachezaji wake na wale wa Ivory Coast huku akipongeza kikosi chake.

"Tulicheza dhidi ya Ivory Coast na wachezaji wengi wa ndani na nimesema mara nyingi kwamba wachezaji katika ligi ya Kenya hawako katika viwango vya kimwili vinavyotarajiwa kucheza dhidi ya aina hii ya timu kubwa. Katika mazingira kama haya, ningesema walifanya vizuri sana..."  Firat alisema