Christiano aliitwa kikosini kwa ubora wake wala si 'kuwa na jina' -Roberto Martinez

Ureno itafungua kampeni yao Jumanne dhidi ya taifa la Czech kuanzia saa nne usiku kwenye mashindano ya Euro 2024.

Muhtasari

•Kocha wa Ureno Roberto Martinez amesema  kuwa alimuita Ronaldo kwenye kikosi cha Ureno kutokana na ubora wake na wala si kuwa na 'jina kubwa'.

•Ronaldo alifunga mabao 50 msimu uliopita na klabu yake ya Al-Nassr na kumaliza kama mfungaji bora.

Christiano Ronaldo
Christiano Ronaldo
Image: Facebook

Kocha wa timu ya taifa ya Ureno, Roberto Martinez amesema kuwa alimuita mshambulizi wa Al-Nassr, Christiano Ronaldo kwenye kikosi hicho kutokana na ubora wake wa kufunga mabao na wala si kuwa na 'jina kubwa '.

Wakati wa mazungumzo na waandishi wa habari, siku ya Jumatatu,Martinez alimtaja Christiano Ronaldo kama baadhi ya wachezaji mahiri kwenye kikosi chake cha Ureno na ambao watawezesha timu hio kufika kiwango bora kwenye mashindano ya Euro 2024.

"Christiano yuko katika timu ya taifa kwa ubora...hakuna anayeingia katika timu ya taifa kwa kuwa na jina tu. Christiano alifunga mabao 50 katika michezo 51 sawia na klabu yake katika ligi yake,na alifunga mabao tisa katika raundi zetu za kufuzu." Roberto Martinez alisema.

Vile vile beki wa kati wa Ureno Ruben Dias alimmiminia sifa tele mshambulizi huyo wa zamani wa Manchester United.

"Anawakilisha kuwa unaweza kuota na ukafanikiwa.Anawakilisha mambo mengi,lakini kikubwa niseme kuwa ni furaha kuwa naye pamoja nasi,zaidi ya haya yote ,madogo,yeye kuwa nasi katika hili....anazidi kuonyesha kuwa anataka kushinda tena na tena ....yeye ni nahodha wetu na tunamfuata  hadi mwisho." Dias alisema.

Ronaldo aliwekwa kwenye benchi na kocha wa zamani Fernando Santos katika mechi zake kuu mbili za mwisho za kimataifa akiwa na Ureno kwenye kombe la dunia la FIFA huko Qatar mnamo 2022.

Ureno itakuwa inalenga kunyakua taji lao la pili kwenye mashindano ya Euro mwaka huu,itakapofungua kampeni yao hii leo  Juni 18 dhidi ya taifa la Czech saa nne usiku.

Taji lao la kwanza walinyakua mwaka 2016 huku wakishindwa na Ubelgiji katika hatua ya 16 bora katika toleo la mwisho la michuano hiyo mwaka wa 2021.