Uhispania wafuzu kwa raundi 16 bora baada ya kuwacharaza Italia 1-0

Riccardo Calafiori alijifunga na kuipa Uhispania ushindi

Muhtasari

•Uhispania walikwangura ushindi baada ya Riccardo Calafiori wa Italia kujifunga katika dakika ya 55

•Italia walikuwa na miguso mitatu pekee kwenye eneo la kisanduku cha wapinzani katika kipindi cha kwanza na hakuna hata shuti moja ilililenga lango la Uhispania.

Uhispania washerehekea bao dhidi ya Italia
Image: HISANI

Timu ya Uhispania ndio mabingwa wa kundi B baada ya kuwacharaza Italia bao moja kwa nunge katika mechi ya Alhamisi.

Uhispania walikwangura ushindi baada ya Riccardo Calafiori wa Italia kujifunga katika dakika ya 55.

Uhispania walionyesha umahiri wa juu kutoka mwanzo ambapo mlinda lango Donnarumma aliudaka mpira wa kichwa kutoka kwa mchezaji Pedri wa Uhispania.

Mchezaji Nico Williams alimpa wakati mgumu beki wa kulia wa Italia Giovanni Di Lorenzo ambapo alikaribia kufunga bao kupitia kichwa kabla ya Donnarumma kuwajibika kwa mara ya pili.

Italia walikuwa na miguso mitatu pekee kwenye eneo la kisanduku cha wapinzani katika kipindi cha kwanza na hakuna hata shuti moja ilililenga lango la Uhispania.

Italia hawakujikaza kisabuni kwenye awamu ya pili ya mechi hiyo kwani Uhispania waliendeleza uhodari wao ambapo mchezaji Pedri alikuwa na nafasi njema ya kufunga kabla ya mlinzi wa Italia, Calafiori, kuwarahisishia kazi na kujifunga.

Kulikuwa na viashiria vya tishio vya mashambulizi ya kasi ila Uhispania ndiyo iliendelea kuongeza nafasi za kufunga  ambapo Pedri na Morata walikaribia tena kufunga huku Uhispania ikisonga katika raundi ya 16 baada ya kushinda mechi mbili kati ya mbili, bila kufungwa.

Italia bado wana nafasi ya kusonga mbele ambapo watakutana na Croatia mnamo Jumatatu wakati Uhispania itapambana na Albania."