Robertson aomba msamaha kwa taifa baada ya Scotland kuondolewa kwenye Euro 2024

Scotland ilipokea kichapo cha 1-0 dhidi ya Hungary usiku wa Jumapili 23 Juni 2024.

Muhtasari

•Robertson ameomba msamaha baada ya Scotland kuondolewa kwenye mashindano ya Euro 2024.

•Hungary iliizaba Scotland 1-0 usiku wa Jumapili baada ya bao la dakika za lala salama kutoka kwa Kevin Csoboth.

Nahodha wa Scotland
Andy Robertson Nahodha wa Scotland
Image: Ghetty images

Nahodha wa timu ya taifa ya Scotland,Andy Robertson ameomba msamaha kwa taifa lake baada ya kuondolewa kwenye mashindano ya Euro 2024.

Scotland ilipokea kichapo cha moja komboa ufe mikononi mwa Hungary kwenye mechi ya mwisho ya hatua ya makundi usiku wa Jumapili.Scotland iliishia kuburura mkia kwenye kundi A kwa alama 1 huku Ujerumani na Switzerland wakifuzu  kwa hatua ya kumi na sita bora.

Bao la dakika ya 100 kutoka kwa Kevin Csoboth mwishoni mwa shambulizi la haraka la Hungary, liliwaweka Scotland kwenye safari yao ya kuelekea nyumbani mapema.

Kwenye mazungumzo na waandishi wa habari baada ya mechi,nahodha  wao,Andy Robertson ameomba msamaha taifa zima kwa kuonyesha mchezo mbovu ndani ya mashindano hayo.

"Usiku wa leo ni bala... Vijana wote wametawaliwa kabisa. Ni juu yetu kuwachukua na hilo litatokea polepole lakini hakika. Nitakachosema ni asante kwa nchi kwa sababu tulihisi kila mtu nyuma yetu na tulijua msisimko wa nyumbani..." Robertson alisema.

Scotland wamekuwa wakiondolewa katika hatua ya makundi ya michuano mikubwa katika michuano yote 12 waliyofuzu, nne kati ya hizo zikiwa ni michuano ya Ulaya.Kwa sasa Scotland wanaungana na Poland ambao waliaga mashindano hivi majuzi.

Aidha nafasi ya Hungary katika awamu ya kumi na sita bora bado haijahakikishwa kwani bado wanahitaji kuorodheshwa kati ya timu nne bora zilizo nafasi ya tatu.Watakuwa wanasubiri hadi mechi za hatua ya makundi kukamilika.