Vinicius Junior kukosa mechi dhidi ya Uruguay kwenye robo fainali ,Copa America

Kwa sasa Vinicius Junior ni wa pili kwenye orodha ya wafungaji bora nyuma ya Lautaro Martinez wa Argentina kwenye kombe la Copa America 2024

Muhtasari

•Vinicius  Junior alionyeshwa kadi ya njano wakati wa mechi kati ya Brazil na Colombia na ya pili kwenye michuano ya Copa America.

•Brazil itachuana na Uruguay kwenye mechi ya robo fainali katika kombe la  Copa America 2024 baada ya kumaliza wa pili,kundi D nyuma ya Colombia

Vinicius Junior akionyeshwa kadi ya njano baada ya kumchezea visivyo James Rodriguez wa Colombia
Vinicius Junior akionyeshwa kadi ya njano baada ya kumchezea visivyo James Rodriguez wa Colombia
Image: Hisani

Nyota wa Brazil,Vinicius Junior hatashiriki kwa mechi ya robo fainali ya Copa America ya Brazil dhidi ya Uruguay.

Nyota huyo wa Real Madrid, 23, alionyeshwa kadi ya pili ya njano ya michuano hiyo katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya Colombia.

Vini,alipewa kadi ya njano kwa kumwangusha James Rodriguez baada ya dakika saba tu za mechi huko Santa Clara, California.

Awali ,mchezaji huyo alipewa kadi ya njano dhidi ya Paraguay katika dakika ya 83 ya ushindi wa 4-1 ,mechi ambayo awali alifunga mara mbili. Sasa atakosa pambano la nane bora dhidi ya Uruguay, litakalofanyika Jumamosi huko Las Vegas.

"Inatokea," kocha mkuu wa Brazil Dorival Junior alisema baada ya kudhibitisha kuwa Vinicius Junior hatashiriki.

“Ulikuwa mchezo muhimu na sikumpumzisha mtu yeyote. Tulianza mchezo vizuri sana. Ilikuwa ya kushangaza sana. Ilikuwa changamoto ya kwanza ya mchezo. Lakini watu wanasema tunapaswa kujifunza kucheza bila nyota wetu wakubwa, kwa hiyo sasa ni wakati. Katika nyakati fulani, hatutakuwa na wachezaji muhimu. Tayari tumempoteza Neymar. Ni wakati kwa wachezaji wengine kuongeza kasi.”

Aidha,Kiungo wa kati wa Colombia Jefferson Lerma atakosa pia mchezo ujao wa timu yake, dhidi ya Panama, baada ya kufungiwa pia kwa mara ya pili katika mashindano hayo.

Vinicius Junior, ameichezea nchi yake mechi 33, akifunga mabao matano. Alifunga mara mbili dhidi ya Paraguay na kukaa nyuma ya Lautaro Martinez wa Argentina pekee katika mbio za kuwania kiatu cha dhahabu cha mashindano hayo.

Hata hivyo Brazil italazimika kutafuta ushindi kwenye mechi hio ya robo fainali itakayochezwa Jumapili asubuhi saa kumi ,saa za afrika mashariki kupitia kwa wachezaji mahiri kama vile Raphinha,Rodrygo na wengineo.