Arteta azungumzia mikakati ya Arsenal kushinda EPL tangu 2004

Arteta amedai kuwa makovu ya msimu uliopita ya kupokonywa kikombe cha EPL yatawasaidia vijana wake kujiboresha zaidi msimu ujao.

Muhtasari

•Arteta amesema kuwa timu yake ipo mbioni kusajili wachezaji bora ili kuboresha kikosi chake zaidi.

•Hata hivyo mkuu huyo wa Arsenal amedai kuwa kwa mchambuzi wa kweli na kulingana na takwimu ,Arsenal ilistahili kushinda taji la Epl la msimu jana.

Mikel Arteta
Kocha wa Arsenal Mikel Arteta
Image: X

Kocha mkuu wa Arsenal Mikel Arteta ameelezea mikakati ambayo timu yake inapanga ili kushinda taji la ligi kuu ya EPL tangu mwaka 2004.

Kwenye mazungumzo na ESPN ,Arteta alisimulia kuwa anawinda kuboresha kikosi chake na kukisuka upya huku akizungumzia kuhusu uhamisho.

"Soko ni gumu,tumekuwa wakali sana na tunajizatiti sana naa tuna wazo wazi kabisa la kile tunachotaka kufanya.Itategemea kupata makubaliano sahihi kwa wakati sahihi."

Aliongeza; "Kuna mambo ambayo tunapaswa kuboresha ,hilo ni hakika na tutajaribu kufanya hivyo."

Mkufunzi huyo alipoulizwa kuhusu kama ilimchukua muda  mrefu kusahau msimu uliopita alisema;

"Sitaki kusahau.Nimeridhika sana na  jinsi timu inavyocheza,jinsi wachezaji wanavyoendelea,kile ambacho timu inatoa,na mwelekeo tulionao kama klabu ya mpira wa miguu.Ila tunahitaji maumivu kama hayo na njaa hiyo ya kufikia kile tunachotaka kufikia kwa sababu ushindani ni wa ajabu na tunahitaji kila mtu kuhisi hivyo ili kufanikisha matokeo bora."

Hata hivyo kocha huyo alisimulia kuhusu msimu uliopita huku akisema kuwa Arsenal ilistahili kushinda ligi kuu ya Uingereza.

"Unapokuwa mchambuzi na kukusanya  takwimu zote na kila kitu ambacho timu ya Arsenal imefanya kwa miezi 11 iliyopita katika ligi kuu ya Uingereza,tulipaswa kushinda.Hivyo ndivyo takwimu zinavyosema." Arteta alisema.

Arsenal wapo kwenye mazungumzo na beki wa timu ya Bologna na raia wa Italia,Riccardo Calafiori japo timu nyingi zimeonyesha ari ya kumsajili beki huyo.

Wababe hao watakuwa wanaanza kampeni yao ya ligi kuu ya Uingereza 24/25 nyumbani dhidi ya Wolves Jumamosi,Agosti 17 kabla ya kuwatembelea Aston Villa Agosti 24.