Kocha Enzo Maresca avunja kimya sababu ya kukubali kibarua kigumu kuinoa Chelsea

“Sababu moja ambayo ilinifanya kukubali kuja hapa [Chelsea] ni kwamba nilishawishika kuwa kikosi ni kizuri sana na kimejaa talanta tupu. Hivyo jambo la muhimu kwa sasa ni kwamba tutakuwa na uwezo wa kuanzisha tamaduni mpya..."

Muhtasari

• Maresca anachukua nafasi ya Muargentina Mauricio Pochettino ambaye aliondoka baada ya kukamilisha msimu mmoja na Chelsea katika kile kilichotajwa kuwa ni makubaliano ya pande zote mbili.

ENZO MARESCA
ENZO MARESCA
Image: CHELSEA TV

Kocha Enzo Maresca amewasili katika uga wa nyumbani wa Chelsea, Stamford Bridge na kufanya kikao chake cha kwanza kabisa na wanahabari akiwa kama kocha wa klabu hiyo ya London.

Muitaliano huyo ambaye alikubali mkataba wa miaka 5 na Chelsea takribani mwezi mmoja uliopita akitokea Leicester City amefichua kwamba anajua kibarua kilichopo mbele yake ni kigumu lakini akasema yuko tayari kwa kila jambo.

Maresca alitaja sababu ya kukubali kuionoa Chelsea akisema kikosi kina vijana wengi wazuri wenye talanta tupu, jambo ambalo kulingana naye litampa fursa nzuri ya kuwapa mafunzo ya haraka kuweza kushindania mataji.

“Nina furaha sana kuwa hapa kama kocha wa Chelsea, itakuwa ni safari ya kusisimua na nina furaha ya kuanza haraka iwezekanavyo. Imekuwa bize sana lakini ndio kawaida na mwanzo mpya wowote, unajaribu kuwafahamu kila mtu katika uwanja wa mazoezi, kuwajua baadhi ya wachezaji waliomo, lakini ukweli ni kwamba hisia hizi ni nzuri sana,” Maresca alisema.

“Sababu moja ambayo ilinifanya kukubali kuja hapa [Chelsea] ni kwamba nilishawishika kuwa kikosi ni kizuri sana na kimejaa talanta tupu. Hivyo jambo la muhimu kwa sasa ni kwamba tutakuwa na uwezo wa kuanzisha tamaduni mpya ambayo itatuendesha kuelekea msimu mpya,” aliongeza.

Katika majira haya ya joto, Chelsea wamefanikiwa kusajili baadhi ya wachezaji wakiwemo beki Tosin Adarabioyo kutoka Fulham, Marc Guiu kutoka Barcelona miongoni mwa majina mengine mapya ambayo Maresca anatarajiwa kuanza mechi ya kujifua nao pindi tu kipute cha Euro 2024 kitakapokamilika wikendi hii.