Euro 2024:Uhispania kumenyana na Ufaransa kwenye nusu fainali ya kwanza

Mshindi kati ya timu hizo mbili amekuwa akinyakua ubingwa wa Ulaya katika michezo yote mitatu ya awali ya hatua ya mtoano kati ya pande zote mbili.

Muhtasari

•Kocha wa Ufaransa,Didier Deschamps  awashtumu mashabiki wanaokerwa na mchezo,huku  akiwataka kutotazama mchezo wao ikiwa unawaudhi.

•Ufaransa itachuana na Uhispania kwenye nusu fainali ya kwanza ya Euro 2024 mwendo wa saa nne usiku.

Uhispania washerehekea bao dhidi ya Italia
Image: HISANI

Mechi ya kwanza ya hatua ya nusu fainali katika mashindano ya bara Ulaya [Euro] itachezwa leo kati ya Ufaransa na Uhispania.

Kocha mkuu wa Ufaransa Didier Deschamps amesema kuwa anatazamia ushindi na wala si kuonyesha mchezo mzuri jinsi wengi wamekuwa wakimkashifu.

"Ikiwa unaboeka na hauvutiwi na mchezo wetu waweza kutazama mechi nyingine,si lazima kututazama .Hii ni mashindano ya bara,na ni ngumu kwa kila mtu..." Deschamps alisema.

Ufaransa itaingia katika mchezo huo ikiwa haijawahi kufunga bao la wazi kwenye mechi tano tangu mashindano yaanze.Mechi ya mwisho waliishia kwenye mashuti ya penalti dhidi ya Ureno baada ya sare tasa.

"Hadi sasa,haijakuwa kama ilivyokuwa hapo awali,lakini tuna uwezo wa kushiriki na kuwafurahisha mashabiki wetu kupitia matokeo,hasa katika kipindi ambacho kimekuwa kigumu kwa nchi yetu."

Kwa upande mwingine Uhispania watakuwa wanajaribu kuwinda  taji hilo ,baada ya kushinda  miaka kumi na mbili iliyopita.

Kwenye mahojiano na wanahabari,Kiungo wa Uhispania Rodri alipoulizwa kuhusu kikosi chao kulinganishwa na kile cha enzi za kina Xavi,Iniesta almaarufu 'golden generation'  alisema kuwa ni mapema mno kulinganisha.

"Tunapaswa kufahamu aina ya timu tuliyonayo na jinsi tunavyofanya kazi kwa bidii na kile tunachohitaji kufanya ili kufikia lengo letu.Tuna mechi ngumu sana dhidi ya mojawapo ya timu bora zaidi katika miaka ya hivi karibuni ambayo itatuletea changamoto." Rodri alisema.

Uhispania wamekuwa katika kiwango bora kwenye Euro 2024, wakishinda michezo yote mitano na kufunga mabao mengi zaidi wakiwa na mabao 11.

Pia wana vijana wawili wa kusisimua zaidi kwenye mashindano, Lamine Yamal na Nico Williams. Lakini licha ya matokeo yao ya kuvutia, Uhispania ilisukumwa na wenyeji Ujerumani katika robo fainali, kabla ya Mikel Merino kufunga kwa kichwa dakika ya 119 kuhitimisha ushindi wa 2-1.

Nani ataibuka na ushindi na kutinga kwenye fainali?