Kocha wa Gor Mahia Neiva aelezea umuhimu wa kombe la Cecafa

K'Ogalo wanatarajiwa kumenyana na Red Arrows ya Zambia Jumatano Julai 10, 2024.

Muhtasari

•Kocha wa Gor Mahia anaamini kuwa mashindano ya  kombe la Cecafa yatamsaidia kukisuka kikosi chake na kuwatathmini wachezaji wake.

•Gor ilishuka nchini Tanzania tayari kwa  mashindano hayo yaliyong'oa nanga hii leo,Julai 9,2024

Leonardo Martins Neiva Kocha wa Gor Mahia
Image: Facebook

Kocha mkuu wa Gor Mahia Leonardo Neiva amefichua kuwa michuano ya kombe la Kagame ya baraza la vyama vya soka Afrika mashariki na kati (CECAFA) 2024 nchini Tanzania itampa fursa ya kuwatathmini wachezaji wake.

K'Ogalo wanatarajiwa kumenyana na Red Arrows ya Zambia siku ya Jumatano kwenye uwanja wa Azam Complex saa 9 alasiri kwa saa za Afrika Mashariki. Neiva ambaye hivi karibuni amechukua usukani wa timu hiyo, alieleza matumaini yake na umuhimu wa michuano hiyo kwa juhudi zake za maandalizi.

"Tunatarajia mashindano yenye ushindani mkubwa Tanzania. Lakini hii inakuja wakati mwafaka kunisaidia kutathmini timu kwani nimejiunga siku chache zilizopita," Neiva alisema.

Kikosi cha wachezaji 25 kilisafiri nchini Tanzania huku Neiva akipanga kukizungusha kikosi chake na kutoa nafasi kwa kila mchezaji kuonyesha uwezo wake.

Gor Mahia walipangwa kundi B, wakikabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa mabingwa wa Zambia, Red Arrows, washindi mara 10 wa ligi kuu ya Sudan, Al Hilal, na Telcom FC ya Djibouti.

Gor  ilinyakua kombe hilo mwaka wa 1985 baada ya kuwashinda wapinzani wao wa kudumu wa ligi kuu AFC Leopards mabao 2-0 na kubeba kombe lao la tatu la Cecafa.

Mara ya mwisho michuano ya kanda hiyo ilipofanyika mwaka 2021 jijini Dar es Salaam, Express Fc ya Uganda iliifunga Nyasa Big Bullets FC kutoka Malawi bao 1-0.

Mshindi wa shindano hilo atapokea zaidi ya Ksh 3 milioni kama zawadi ya pesa na kuongeza motisha kwa timu zote zinazohusika.